Kwingineko

Ulinzi waimarishwa mechi ya England na Argentina

ATLANTA: Mamlaka za usalama jijini Atlanta, Marekani, zimetangaza kuimarisha ulinzi kuelekea mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia kati ya England na Argentina utakaochezwa Jumatano.

Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na ukubwa wa mchezo huo na historia ndefu ya ushindani kati ya mataifa hayo mawili, ambayo pia yaliwahi kupigana Vita vya Falkland mwaka 1982.

Polisi wa Atlanta wamesema askari na rasilimali zaidi zimetumwa katika uwanja, maeneo ya burudani na sehemu zenye mikusanyiko mikubwa ili kuhakikisha usalama wa mashabiki na wageni.

England inawania kutinga fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1966, huku Argentina ikisaka kutetea ubingwa wake wa dunia. Mchezo huo pia unatarajiwa kushuhudia Lionel Messi akiikabili England kwa mara ya kwanza akiwa na timu ya taifa katika Kombe la Dunia.

Katika kuelekea mchezo huo, Shirikisho la Wastaafu wa Vita vya Falkland nchini Argentina limewataka mashabiki kutenganisha siasa na michezo, likisisitiza kuwa pambano hilo linapaswa kubaki ndani ya uwanja wa mpira.
Naye kipa wa England, Jordan Pickford, amesema mchezo huo ni wa soka pekee na anaamini matokeo yataamuliwa na kiwango kitakachoonyeshwa uwanjani, si historia ya kisiasa kati ya nchi hizo.

Wakati huo huo, polisi nchini Uingereza wamewasifu mashabiki waliokwenda Marekani kwa mwenendo wao mzuri, lakini wamewataka waliobaki nyumbani kujizuia kufanya fujo baada ya zaidi ya watu 100 kukamatwa kufuatia vurugu zilizotokea wakati wa ushindi wa England dhidi ya Norway kwenye robo fainali.
MWISHO

Related Articles

Back to top button