Manqoba: Nimekuja kuifanya Yanga itawale Afrika

DAR ES SALAAM: Kocha mpya wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amesema amekuja ndani ya klabu hiyo kutimiza ndoto ya kuifanya itawale soka la Afrika, akieleza kuwa lengo lake kuu ni kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).
Kupitia mtandao wake, amesema ameifuatilia Yanga kwa muda mrefu na anatambua ukubwa wa klabu hiyo, jambo lililomfanya kuvutiwa na changamoto ya kuiongoza.
“Lengo langu kubwa ni kushinda Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga ni klabu kubwa ambayo nimekuwa nikiifuatilia kwa muda mrefu na ninafurahia kuwa sehemu yake,” amesema.
Mbali na mafanikio ya kimataifa, kocha huyo amesema ataendelea kulinda heshima ya Yanga katika mashindano ya ndani, akiahidi kuiongoza kutwaa ubingwa wa sita mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alikiri kuwa kupoteza Kombe la Shirikisho la CRDB msimu uliopita kulikuwa pigo kwa klabu hiyo, lakini akaweka wazi kuwa atahakikisha kombe hilo linarejea Jangwani msimu ujao.
Pia, amewapongeza viongozi wa Yanga kwa kutekeleza maombi yake ya usajili, akisema wachezaji wenye ubora aliohitaji watasaidia kutekeleza falsafa yake ya soka.




