Habari Mpya

Kiungo wa Afrika Kusini Jayden Adams afariki dunia

JOHANNESBURG: Soka la Afrika Kusini limegubikwa na majonzi kufuatia kifo cha kiungo wa klabu ya Mamelodi Sundowns na timu ya taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana), Jayden Adams, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 25.

Adams amefariki siku chache baada ya kuisaidia Afrika Kusini katika fainali za Kombe la Dunia 2026, ambapo alicheza mechi tatu za hatua ya makundi.

Kiungo huyo alianza katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Mexico uliomalizika kwa Afrika Kusini kufungwa mabao 2-0, kisha akaanza tena dhidi ya Czechia katika sare ya 1-1 kabla ya kuingia akitokea benchi kwenye ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Korea Kusini. Hakushiriki mchezo wa hatua ya 32 bora dhidi ya Canada ambao Bafana Bafana ilipoteza kwa bao 1-0.

Waziri wa Michezo wa Afrika Kusini, Gayton McKenzie, amesema taifa limepoteza mmoja wa vipaji vikubwa vya soka.

“Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa za kifo cha Jayden Adams. Soka la Afrika Kusini limepoteza mmoja wa wachezaji wake wenye vipaji vikubwa, na taifa linaomboleza pamoja na familia yake, wachezaji wenzake na mamilioni ya mashabiki waliomshuhudia akikua kutoka akademi hadi kuwa nyota wa Bafana Bafana,” amesema McKenzie.

Adams alianza safari yake ya soka kupitia akademi ya Stellenbosch FC na kuwa mchezaji wa kwanza kutoka akademi hiyo kusaini mkataba wa timu ya wakubwa. Aliichezea Stellenbosch mechi 139 na kusaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Carling Knockout mwaka 2023.

Mwezi Januari 2025 alijiunga na Mamelodi Sundowns, ambako aliendelea kung’ara na kujihakikishia nafasi katika kikosi cha timu ya taifa.

Chama cha Wachezaji wa Soka Afrika Kusini (SAFPU) pia kimetoa salamu za rambirambi kikisema kifo cha Adams ni pigo kubwa kwa familia yake, klabu zake, timu ya taifa na soka la Afrika Kusini kwa ujumla.

Hadi sasa, chanzo cha kifo cha Jayden Adams hakijawekwa wazi.

Related Articles

Back to top button