AFCON

Samatta aaga, wadau wamsihi asubiri Afcon

DAR ES SALAAM: UAMUZI wa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kutangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa umeibua hisia na maoni mbalimbali kutoka kwa viongozi wa Serikali, wadau wa soka na wachezaji, wengi wao wakimtaka afikirie upya kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Miongoni mwa waliotoa maoni yao ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwanafa’, ambaye alimshukuru Samatta kwa mchango wake mkubwa huku akimuomba arejee kwenye uamuzi huo ili aiongoze Tanzania katika fainali za AFCON zitakazofanyika nchini mwakani.

“Nahodha, asante kwa kila kitu, asante sana. Hudaiwi na mtu. Tuna ombi moja tu watu wa mpira, hatuwezi kushiriki AFCON itakayopigwa nyumbani pamoja? Ukiwa dimbani. Halafu tukujengee mnara wako mkubwa tuache upumzike, tafadhali. Na asante sana Nahodha,” aliandika Mwinjuma.

Kwa upande wake, Meneja Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, naye alimsihi Samatta abadili uamuzi wake akisisitiza kuwa taifa bado linamhitaji.

“Lala ukiamka kunywa chai halafu ufute hii kepsheni. Taifa linakuhitaji kwenye AFCON yetu ya kihistoria mwakani. Tutaagana uwanjani, si Instagram,” aliandika Kamwe.

Ujumbe huo pia uliungwa mkono na mshambuliaji wa Twiga Stars Aisha Masaka, ambaye amesema “Vijana wengi tumefanikisha ndoto zetu kwa kukuangalia wewe kama mfano. Asante kwa kila kitu , wewe ni mkongwe wa kweli,”

Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Samatta amesema amefikia uamuzi huo baada ya kutafakari kwa kina, akitangaza rasmi kustaafu kuitumikia Taifa Stars baada ya safari ya takribani miaka 15.

Amesema miaka 10 aliyokuwa nahodha wa timu hiyo imebeba mafanikio makubwa, ikiwemo kuiongoza Tanzania kufuzu fainali za AFCON mara tatu na kuweka historia ya kufika hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza.

Samatta amesema anaamini umefika wakati wa kizazi kipya cha wachezaji kupewa nafasi ya kuendelea kuipeleka Tanzania kwenye mafanikio makubwa zaidi.

Related Articles

Back to top button