World Cup

Hossam: FIFA inamlinda Messi

...ataja fedha kuwa sababu kubwa

ATLANTA: Kocha Mkuu wa Misri, Hossam Hassan, amelishutumu Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa kile alichodai kuwa linalinda maslahi yake kwa kuhakikisha nahodha wa Argentina, Lionel Messi, anaendelea kubaki kwenye Kombe la Dunia la 2026.

Hossam alitoa kauli hiyo kwa hasira baada ya Misri kuondolewa katika hatua ya 16 bora kufuatia kupoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya mabingwa watetezi, Argentina, katika mchezo uliogubikwa na maamuzi yaliyozua mjadala mkubwa.

Akizungumza baada ya mechi, Hassan alisema timu yake imeonewa na kunyimwa haki, akisisitiza kuwa Misri ndiyo iliyostahili kusonga mbele kutokana na kiwango ilichoonyesha uwanjani.

“Yote yanahusu fedha. Wanataka Messi aendelee kuwepo kwenye mashindano. Katika soka, mambo mengi hutokea nje ya uwanja kwa sababu ya maslahi mbalimbali. Kilichotokea hakikuwa cha haki. Misri ilistahili kufuzu. Sisi ndiyo tulikuwa timu bora,” alisema Hossam.

Kocha huyo alieleza kuwa bado haelewi kwa nini haki haikutendeka katika mchezo huo, akidai kuwa timu yake imepitia dhuluma ambayo haipaswi kuvumiliwa katika soka la kimataifa.

“Kwa nini hakuna haki katika michezo? Sitaki kutumia maneno mazuri kuficha ukweli. Leo tumetendewa isivyo haki. Tumepitia dhuluma. Hii ndiyo njia yangu ya kuzungumza na kusimamia ninachoamini. Sitatazama tena mechi yoyote katika mashindano haya, aliongeza.

Mbali na malalamiko hayo, Hassan alidai kuwa kulikuwa na shinikizo kutoka upande wa Argentina ambalo, kwa mtazamo wake, liliathiri mwenendo wa mchezo.

“Inaonekana kulikuwa na shinikizo kutoka upande wa Argentina kuhusu matokeo haya. Katika soka, wakati mwingine kuna mambo yanayotokea nje ya uwezo wa kiufundi. Mabingwa wa dunia walipata uungwaji mkono katika kila ngazi,” alisema.

Katika mchezo huo, Misri ilianza vyema na hata kufanikiwa kupata bao ambalo baadaye lilibatilishwa kwa uamuzi wenye utata.

Iliongoza mabao mawili kabla ya Argentina kufanya mabadiliko na kufunga mabao matatu ndani ya dakika 15 za mwisho na kuibuka na ushindi wa 3-2.

Hossam pia alipinga bao la ushindi la Enzo Fernández, akidai kuwa kabla ya bao hilo, mshambuliaji Mohamed Salah alistahili kupewa penalti, lakini waamuzi waliamua kuendelea na mchezo, jambo ambalo lilichangia kuiumiza ya timu yake na kumaliza safari ya Misri katika Kombe la Dunia 2026.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button