Waamuzi wa Kuogelea Kukutana Dar kuboresha Ufanisi

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Michezo ya Maji Afrika kwa kushirikiana na Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) limeandaa kliniki maalumu ya mafunzo kwa waamuzi na maofisa wa kiufundi wa mchezo wa kuogelea yenye lengo la kuongeza ujuzi na kuboresha viwango vya usimamizi wa mashindano barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TSA, mafunzo hayo yatafanyika kwa siku mbili, Julai 11 na 12, 2026, katika Hoteli ya Colosseum jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa waandaaji, kliniki hiyo itawakutanisha maofisa wa kiufundi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika ili kupata maarifa mapya, kubadilishana uzoefu na kuimarisha uwezo wa kusimamia mashindano kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Mwezeshaji mkuu wa mafunzo hayo atakuwa Max Kanyerezi, ambaye atatoa mafunzo kuhusu mbinu za kisasa za uamuzi na usimamizi wa mashindano ya kuogelea.
Waandaaji wamesema kuwa kuendelea kuwajengea uwezo maofisa wa kiufundi ni hatua muhimu katika kukuza mchezo wa kuogelea na michezo mingine ya maji barani Afrika, huku wakisisitiza kuwa ubora wa waamuzi ni msingi wa mashindano yenye haki na viwango vya kimataifa.




