Kane: Najivunia imani iliyooneshwa na wachezaji wenzangu

GEORGIA: Nahodha wa England, Harry Kane amesema anajivunia imani na moyo wa kupambana uliooneshwa na wachezaji wenzake baada ya kuiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya DR Congo na kutinga hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia.
Kane aliibuka shujaa wa England kwa kufunga mabao mawili ndani ya dakika 11, baada ya Brian Cipenga kuifungia DR Congo bao la mapema katika dakika ya saba ya mchezo.
Akizungumza baada ya mechi, Kane alisema walifahamu tangu mwanzo kuwa wangekutana na upinzani mkali kutoka kwa DR Congo, ambayo ilicheza kwa nidhamu kubwa ya kujilinda huku ikitumia vyema mashambulizi ya kushtukiza.
“Ninajivunia kundi hili na wachezaji wenzangu. Tulizungumza kabla ya mchezo kuhusu ugumu wa mechi hii. Walituonyesha ubora wao hasa katika dakika za mwanzo, lakini tuliendelea kuamini na kupambana hadi mwisho,” alisema Kane.
Nahodha huyo alisema England ilianza kucheza vizuri zaidi baada ya dakika 25, huku ikitengeneza nafasi nyingi za kufunga, ingawa kipa wa DR Congo aliokoa mipira kadhaa iliyokuwa ikielekea wavuni.
“Ulianza kuhisi huenda siku isiwe yetu kutokana na namna kipa wao alivyokuwa akiokoa. Lakini tuliendelea kuamini, tukaendelea kupeleka mipira kwenye maeneo sahihi, na nilijua mmoja wetu angekuwa shujaa wa mchezo. Nashukuru leo imekuwa zamu yangu,” aliongeza.
Kwa ushindi huo, England imefuzu hatua ya 16 bora na sasa itamenyana na Mexico, huku Kane akiwataka wachezaji wenzake kufurahia ushindi huo kabla ya kuanza maandalizi ya mchezo unaofuata.




