Filamu

Wahadzabe Wanogesha Tamasha la ZIFF 2026

ZANZIBAR:WASHIRIKI kutoka kabila la Wahadzabe wamekuwa kivutio kikubwa katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF 2026), baada ya kuonesha utamaduni wao wa kipekee uliovutia mamia ya wageni waliohudhuria tamasha hilo visiwani Zanzibar.

Wahadzabe hao, waliowasili kutoka Mkoa wa Arusha, walipata fursa ya kuonesha baadhi ya mila, desturi na mbinu zao za maisha ya asili, hali iliyowavutia washiriki wengi wa tamasha hilo kutoka ndani na nje ya Tanzania. Wageni walionekana kuwa na hamu kubwa ya kujifunza kuhusu historia, maisha na utamaduni wa jamii hiyo maarufu kwa maisha ya uwindaji na ukusanyaji.

Akizungumza katika tamasha hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hamza Hassan Juma, alisema uwepo wa Wahadzabe ni sehemu ya utalii wa kiutamaduni unaoifanya Zanzibar kuwa kitovu cha kukutanisha watu wa tamaduni mbalimbali kutoka Tanzania na duniani kote.

Alisema tamasha la ZIFF limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonesha utofauti wa tamaduni zilizopo nchini, huku likiwapa wageni nafasi ya kujifunza na kuthamini urithi wa makabila mbalimbali ya Tanzania. Aidha, aliipongeza ZIFF kwa kuendelea kutumia sanaa na filamu kama nyenzo ya kuimarisha umoja na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Washiriki wengi waliohudhuria tamasha hilo walieleza kufurahishwa na uwepo wa Wahadzabe, wakisema umetoa sura tofauti na ya kipekee katika ZIFF 2026. Wengi walitumia fursa hiyo kujifunza kuhusu maisha yao ya jadi, jambo lililoifanya jamii hiyo kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya tamasha la mwaka huu.

Related Articles

Back to top button