Ally: Dar City tulikuwa bora kuliko JKT

DAR ES SALAAM: MCHEZAJI wa Dar City, Ally Abdallah, amesema wanafurahia ushindi wa pointi 62-33 walioupata dhidi ya JKT kwa kuwa wapinzani wao ni miongoni mwa timu zinazowapa ushindani mkubwa kila wanapokutana katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mchezo huo uliochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Don Bosco, Oysterbay, Ally amesema licha ya JKT kujitahidi kutumia uwezo wao wote, Dar City ilikuwa bora zaidi katika mchezo huo.
“Ushindi dhidi ya JKT tunaufurahia na una maana kubwa kwa sababu ni moja ya timu zinazotupa upinzani kila tunapocheza nao katika ligi ya ndani. Wapinzani walijitahidi kwa uwezo wao, lakini sisi tulikuwa bora kuliko wao,” amesema Ally.
Kwa upande wake, mchezaji wa JKT, Jackson Brown, amesema Dar City haipaswi kubezwa ni timu nzuri huku akieleza sababu za kupoteza ni kutokana na uchanga wa wachezaji walionao kuna vijana wengi wapya huku baadhi ya wachezaji wakongwe wakiwa kwenye majukumu mbalimbali ya Jeshi.
“Dar City ni timu iliyokamilika kila sekta tofauti na sisi tuna vijana wengi wageni na wale wakongwe wapo kwenye majukumu mbalimbali ya Jeshi. Hata hivyo, muda si mrefu tutakuwa imara zaidi baada ya wengi kurejea,” amesema Brown.




