Haaland ang’ara Norway ikiichapa Iraq 4-1

FOXBOROUGH: NAHODHA na mshambuliaji hatari wa Norway, Erling Haaland, ameanza vyema kampeni yake ya kwanza ya Kombe la Dunia baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Iraq kwenye mchezo wa Kundi I uliochezwa usiku wa kuamkia leo.
Haaland, mwenye umri wa miaka 25, alikuwa kivutio kikubwa kabla ya mchezo huo na alithibitisha ubora wake kwa kuiongoza Norway kupata ushindi katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia tangu mwaka 1998.
Norway ilianza kupata bao la kuongoza kabla ya Iraq kusawazisha dakika 10 baadaye kupitia mshambuliaji wake Aymen Hussein, aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Amir Al Ammari.
Hata hivyo, furaha ya Iraq haikudumu kwa muda mrefu baada ya Haaland kutumia makosa ya kipa Jalal Hassan. Kipa huyo alichelewa kuondoa mpira na badala yake akampiga Haaland, huku mpira ukimgonga goti mshambuliaji huyo na kuingia wavuni.
Bao hilo lilikuwa la 57 kwa Haaland katika mechi 51 za kimataifa akiwa na Norway, akiendelea kuthibitisha uwezo wake mkubwa wa kufumania nyavu.
Iraq walionesha upinzani mkubwa na kutengeneza nafasi kadhaa, lakini Norway walirejea kipindi cha pili kwa nguvu zaidi. Beki Leo Ostigard aliifungia Norway bao la tatu dakika ya 76 kabla ya Aymen Hussein kujifunga katika dakika za nyongeza na kuhitimisha ushindi wa mabao 4-1.
Baada ya mchezo huo, Haaland alisema ushindi huo ni mwanzo mzuri lakini alionya kuwa mechi zijazo zitakuwa ngumu zaidi.
“Mechi zijazo zitakuwa ngumu kuliko hii. Tunapaswa kucheza vizuri zaidi,” amesema Haaland.
Kwa upande wake, kocha wa Iraq, Graham Arnold, amewasifu wachezaji wake licha ya kipigo hicho, akisema makosa machache yaliigharimu timu yake.
Katika mchezo ujao wa Kundi I, Norway itavaana na Senegal mchezo ujao, huku Iraq ikikabiliwa na mtihani mgumu dhidi ya Ufaransa.




