Kwingineko

FIFA yatetea Visa, bei za Tiketi kuelekea Kombe la Dunia 2026

MEXICO: SHIRIKISHO la Soka Duniani (FIFA) limetetea uamuzi wake kuhusu bei za tiketi na namna masuala ya visa yanavyoshughulikiwa kuelekea kuanza rasmi kwa Kombe la Dunia 2026, huku mashindano hayo yakianza leo kwa mchezo wa ufunguzi kati ya Mexico na Afrika Kusini.

Mashindano ya mwaka huu yanayoandaliwa kwa pamoja na Marekani, Mexico na Canada yanaingia kwenye historia kama Kombe la Dunia kubwa zaidi kuwahi kufanyika, yakishirikisha timu 48 na jumla ya michezo 104 itakayochezwa kwa kipindi cha karibu wiki sita hadi fainali ya Julai 19 itakayopigwa kati amji wa New Jersey nchini Marekani.

Pamoja na matarajio ya kuvunja rekodi ya mapato kwa kukusanya takribani dola bilioni 13, FIFA imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka kuhusu gharama kubwa za tiketi, huku baadhi ya tiketi zikiripotiwa kufikia zaidi ya dola 30,000.

Akizungumza jijini Mexico City siku moja kabla ya kuanza kwa mashindano hayo, Rais wa FIFA, Gianni Infantino, alitetea mfumo wa upangaji wa bei akisema shirika hilo limezingatia uwezo wa mashabiki wa kawaida.

Infantino alisema pamoja na kuwepo kwa tiketi za bei ya juu, bado kulikuwa na tiketi za kuanzia dola 60 kwa ajili ya kuwapa nafasi mashabiki wengi zaidi kushiriki mashindano hayo.

Alisisitiza kuwa kwa wastani wa bei za tiketi katika michezo mikubwa ya Marekani, tiketi za Kombe la Dunia bado zinaendelea kuwa miongoni mwa zenye gharama nafuu zaidi.

Mbali na suala la tiketi, FIFA pia imezungumzia changamoto zilizojitokeza kwenye utoaji wa visa baada ya baadhi ya wageni na viongozi kushindwa kuingia Marekani kuelekea mashindano hayo.

Miongoni mwa matukio yaliyozua mjadala ni kushindwa kwa mwamuzi kutoka Somalia, Omar Artan, kuruhusiwa kuingia Marekani baada ya mamlaka za uhamiaji kueleza kuwepo kwa masuala ya kiusalama yaliyohitaji uchunguzi zaidi.

Akizungumzia suala hilo, Infantino alisema si kila jambo lipo ndani ya uwezo wa FIFA na kusisitiza kuwa wakati mwingine ni muhimu kutoa muda kwa mamlaka husika kufanya kazi zao badala ya kutoa hukumu za haraka.

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo wa FIFA amesema ushiriki wa Iran kwenye mashindano hayo licha ya mazingira magumu ya kisiasa ni ishara kuwa soka linaendelea kuwa jukwaa la kuunganisha watu na mataifa.

Kombe la Dunia 2026 linaanza rasmi leo huku mamilioni ya mashabiki duniani wakisubiri kushuhudia historia mpya ya mashindano hayo makubwa zaidi ya soka kuwahi kuandaliwa duniani.

Related Articles

Back to top button