Mastaa

Aliyeshinda ndege ya Mr. Beast akamatwa

PARAGUAY:MAMBO yaligeuka filamu kwa rubani maarufu mwenye asili ya Jamaica na Marekani, Jabari Stephan Brown maarufu kama ‘Captain Treezy’, baada ya kukamatwa nchini Paraguay kuhusishwa na uchunguzi wa dawa za kulevya wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 466.

Brown, ambaye alipata umaarufu mkubwa duniani baada ya kushinda ndege binafsi kwenye shindano la YouTuber maarufu MrBeast mwaka 2025, alijikuta mikononi mwa polisi mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya mamlaka kumhusisha na ndege iliyokutwa ikiwa imebeba zaidi ya kilo 260 za bangi yenye kiwango kikubwa cha kemikali ya THC.

Taarifa kutoka Paraguay zilieleza kuwa rubani huyo alikamatwa katika hoteli moja jijini Asunción huku wachunguzi wakifuatilia mtandao wa usafirishaji wa dawa hizo ambao thamani yake mitaani inakadiriwa kufikia dola milioni 3.6 za Marekani.

Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa kina kufanyika, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ilibaini kuwa Brown hakuwa na uhusiano wowote na biashara hiyo haramu. Mamlaka zilieleza kuwa alishirikiana kikamilifu katika uchunguzi na hakufahamu chochote kuhusu mzigo haramu uliokuwa ndani ya ndege hiyo.

Wakati Brown akiondolewa katika tuhuma hizo, watu wengine watatu walibaki mikononi mwa sheria na kufunguliwa mashtaka kuhusiana na sakata hilo.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa ndege iliyohusishwa na tukio hilo ilisafiri kutoka Miami kupitia Panama kabla ya kutua Paraguay, huku rubani mkuu wa safari hiyo akidaiwa kuondoka nchini humo kabla ya operesheni ya ukamataji kufanyika.

Captain Treezy alijizolea umaarufu mkubwa Desemba mwaka 2025 baada ya kuibuka mshindi katika shindano la MrBeast la ‘100 Pilots Fight For A Private Jet’, ushindi uliomzawadia ndege ya kifahari aina ya Hawker 400XP yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 310.

Mamlaka zimeweka wazi kuwa ndege aliyoshinda kutoka kwa MrBeast haihusiani kwa namna yoyote na uchunguzi wa dawa za kulevya unaoendelea.

Baada ya kuachiwa huru, Brown alitumia mitandao ya kijamii kueleza kuwa amekuwa akimtegemea Mungu katika nyakati ngumu na kusisitiza kuwa hana hatia katika sakata hilo. Mashabiki wake nao walimiminika mtandaoni kusherehekea kuachiwa kwake huku wakimpa maneno ya faraja baada ya kupitia kipindi kigumu kilichotikisa jina lake duniani.

Related Articles

Back to top button