AFCON

Wavu kutumika kutangaza AFCON 2027

DAR ES SALAAM: OFISA Michezo Mwandamizi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu, amewahamasisha Watanzania kutumia Mashindano ya Mpira wa Wavu Ufukweni Afrika Kanda ya Tano kama jukwaa la kuitangaza Tanzania kuelekea mashindano ya AFCON 2027.

Maguzu ametoa kauli hiyo jana wakati wa ufunguzi rasmi wa mashindano hayo yanayofanyika katika Fukwe ya Sawa Sawa jijini Dar es Salaam, yakizikutanisha timu kutoka mataifa sita ya Afrika.

Amesema mashindano hayo ni sehemu ya kuonesha uwezo wa Tanzania kuandaa matukio makubwa ya kimataifa sambamba na kutangaza vivutio vya nchi na sekta ya michezo.

“Tunapaswa kutumia mashindano haya kuitangaza Tanzania na maandalizi ya AFCON 2027, ambayo nchi yetu ni miongoni mwa waandaaji,” amesema Maguzu.

Pia, amekipongeza Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TVF) kwa maandalizi mazuri yaliyowezesha kufanyika kwa mashindano hayo ya kimataifa.

Mashindano hayo yameanza rasmi Mei 21 na yanatarajiwa kuendelea hadi Mei 25 mwaka huu yakishirikisha nchi za Tanzania, Burundi, Kenya, Uganda, Misri na Sudan.

Michuano hiyo inahusisha timu za wanawake na wanaume zinazowania nafasi za kufuzu mashindano ya Afrika kupitia ukanda wa CAVB
Zone V pamoja na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2028 itakayofanyika Los Angeles, Marekani.

Kwa mujibu wa waandaaji, mashindano hayo pia yana lengo la kukuza mchezo wa mpira wa wavu ufukweni nchini na kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia michezo.

Related Articles

Back to top button