
KIGOMA: KOCHA Mkuu wa Mashujaa FC, Jamhuri Kihwelu amesema hana hofu na Simba kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa kesho, akisisitiza timu yake ipo tayari kupambana kutafuta ushindi.
Kihwelu amesema uzoefu wake ndani ya Simba unampa uelewa mkubwa wa mazingira ya klabu hiyo, licha ya kutofuatilia mechi zao za hivi karibuni.
“Hii ligi Simba nilikuwa mchezaji nikaja nikawa kocha. Nawafahamu Simba lakini siwafahamu wachezaji wao wala mechi zao za ligi sijawahi kuziona, lakini kwa sababu tuko kwenye ushindani tutapambana tu. Siogopi Simba wala nani, ni timu kubwa na nawaheshimu lakini Mashujaa ni timu kubwa vilevile,” amesema Kihwelu.
Amesema malengo yao ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri ili kuendelea kujisitiri katika msimamo wa ligi.
Kwa upande wa Simba, Kocha Msaidizi Seleman Matola amesema kikosi hicho kimejiandaa vizuri kuhakikisha kinaondoka na pointi tatu licha ya kutambua ugumu wa mchezo huo.
“Pamoja na ugumu na ubora wao, tumejiandaa kupata alama tatu katika mchezo huo. Maandalizi ni mazuri sana. Kinachotupa jeuri baadhi ya wachezaji wetu waliokuwa majeruhi wameanza kurudi,” amesema Matola.
Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi na pointi 49 baada ya kucheza michezo 22, huku Mashujaa ikiwa nafasi ya tisa na pointi 26 baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.
Katika mchezo wa raundi ya kwanza, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mashujaa.
Takwimu zinaonesha Simba ipo kwenye kiwango kizuri baada ya kushinda michezo minne na kutoka sare mmoja katika mechi tano zilizopita, huku Mashujaa ikishinda mchezo mmoja na kutoka sare nne.
Katika rekodi ya jumla ya timu hizo kukutana mara sita, Simba imeibuka na ushindi mara tano huku Mashujaa ikishinda mchezo mmoja pekee.




