Kuogelea

Taliss IST yatwaa Ubingwa wa Kuogelea Taifa

DAR ES SALAAM: KLABU ya Taliss IST imeibuka bingwa wa Mashindano ya 18 ya Kuogelea ngazi ya Klabu baada ya kujikusanyia pointi nyingi zaidi katika michuano hiyo iliyohitimishwa jana katika Bwawa la Kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika.

Katika matokeo ya jumla, Taliss IST ilitwaa ubingwa kwa kujikusanyia alama 448.5, ikifuatiwa na Dar Swim Club iliyoshika nafasi ya pili kwa alama 320.5. Mwanza Swimming Club ilimaliza katika nafasi ya tatu kwa alama 133 huku Reptide Swimming Club ikishika nafasi ya nne kwa alama 129.5.

Washiriki waliofanya vizuri walitunukiwa medali na zawadi mbalimbali zilizotolewa na Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA).

Akizungumza baada ya mashindano hayo, Mkurugenzi wa Ufundi wa TSA, Amina Mfaume, amesema mashindano hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kitaalamu, huku waogeleaji wengi wakiboresha na hata kuvunja rekodi zao binafsi.

Amesema mafanikio hayo ni ishara njema kuelekea mashindano ya kimataifa yanayokuja, ikiwemo michuano ya CANA Zone itakayofanyika nchini Uganda pamoja na Mashindano ya Dunia yatakayofanyika China baadaye mwaka huu.

Mwenyekiti wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) David Mwasyoge amesema jumla ya vijana 200 wameshiriki mashindano hayo na kwamba wanajivunia idadi ya vijana kuendelea kuongezeka na kufanya vizuri.

Kwa upande wake, Kocha wa kuogelea Thobias Mangunga amesema wanachojivunia katika mashindano hayo ni vijana wengi kuimarisha muda wa kuogelea na kuvunja rekodi mbalimbali hatua inayoonesha wazi kuwa kuna mwelekeo wa kufanya vizuri baadaye.
Mwisho

Related Articles

Back to top button