Nyumbani

Rais Mwinyi atoa ahadi kwa Simba kabla ya fainali dhidi ya RS Berkane

ZANZIBAR: RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameonesha mshikamano na uzalendo wa hali ya juu kwa klabu ya Simba SC kwa kuahidi kuhudhuria fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane kutoka Morocco.

Mchezo huo wa kihistoria unatarajiwa kufanyika Mei 25, 2025, saa 10:00 alasiri katika Uwanja mpya wa kisasa wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa Morocco, Simba walilazimika kupokea kichapo cha mabao 2-0. hivyo, kwa mkondo wa pili, Simba wanahitaji ushindi wa mabao 3-0 ili kutwaa taji hilo la kifahari barani Afrika.

Kupitia taarifa rasmi iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu ya Zanzibar, Raqey Mohamed, imeelezwa kuwa Rais Mwinyi ataungana na Watanzania wengine katika kutoa sapoti ya nguvu kwa wawakilishi hao wa taifa.

Uwepo wake uwanjani unatarajiwa kuwa chachu ya ushindi na motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi la Simba kuhakikisha kombe hilo linabaki katika Ardhi ya Tanzania.

Zaidi ya hayo, Rais Mwinyi ametangaza zawadi maalum kwa Simba kwa kuigharamia gharama zote za matumizi ya Uwanja wa New Amaan Complex kwa ajili ya fainali hiyo. Hii inaonyesha dhamira yake ya kweli katika kuendeleza michezo nchini na kulipa hadhi soka la Tanzania katika jukwaa la kimataifa.

“Uamuzi huu wa Rais Mwinyi unalenga kuonesha mapenzi yake kwa michezo na kuhamasisha ushindi wa Simba kwenye mechi hii ya kihistoria,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za kuinua michezo, hasa katika nyanja za kimataifa.

Fainali hiyo inatarajiwa kuvuta maelfu ya mashabiki kutoka ndani na nje ya nchi, huku matarajio makubwa yakiwa kwa Simba kutengeneza historia mpya ya soka la Tanzania.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button