Mastaa

Zuchu: Siri ya mafanikio ni kazi na Mungu mbele

DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Zuhura Othuman maarufu kama Zuchu, amewatia moyo mabinti wanaotamani kuingia katika tasnia ya burudani, akiwahimiza kutokata tamaa bali kufanya kazi kwa bidii, kuwa na nidhamu na kumtanguliza Mungu katika safari yao ya mafanikio.

Zuchu amesema mafanikio katika tasnia ya burudani yanawezekana kwa mtu yeyote mwenye ndoto, akisisitiza kuwa siri kubwa ni kuchanganya bidii katika kazi na kumtegemea Mungu.

Akizungumza na mabinti wanaotamani kujenga majina yao katika tasnia ya burudani, hususan muziki, msanii huyo amesema hakuna sababu ya kujiona hawawezi kufanikiwa kutokana na changamoto wanazokutana nazo mwanzoni mwa safari zao.

“Mimi nikupe moyo, inawezekana kuwa mkubwa kwa combination ya vitu hivi viwili: kazi sana na Mungu mbele,” amesema Zuchu.

Amesisitiza kuwa wanaoanza safari ya muziki wanapaswa kujifunza kuthamini hatua ndogo wanazopiga badala ya kujilinganisha na wasanii wengine ambao tayari wamepiga hatua kubwa.

Amesema hata msanii anapokuwa na mashabiki watano tu, anapaswa kuhakikisha anawapa burudani na kuwathamini, huku akiendelea kutangaza kazi zake kupitia majukwaa mbalimbali.

“Kama una audience watano, wafurahishe hao hao. Usiangalie mwenzangu anapata kumi eti nivunjike moyo kwa sababu nina watano. Hapo hapo ulipo, hiyo hiyo simu yako, hizo hizo content zako kila siku hakikisha una-promote kazi yako,” amesisitiza.

Aidha, Zuchu amebainisha kuwa nidhamu ya kazi ni msingi mwingine muhimu unaoweza kumfikisha msanii kwenye mafanikio makubwa, akiwataka mabinti kutokubali changamoto za mwanzo kuwakatisha tamaa.

Kwa mujibu wa msanii huyo, mchanganyiko wa kufanya kazi kwa juhudi, kuwa na nidhamu na kumtanguliza Mungu ndiyo misingi iliyomsaidia kufika hatua aliyonayo sasa.

“Kingine, nidhamu ya kazi yako itakupa mafanikio makubwa mno. Asikuongopee mtu, hii combination ndiyo iliyonisimamisha mimi hadi leo nipo hapa. Hakuna anayefanikiwa kwa bahati mbaya,” amesema.

Ameongeza kuwa anacholenga ni kuwapa moyo mabinti ambao huenda wanapoangalia mazingira yao ya sasa wanaona ndoto zao haziwezi kutimia, akiwahakikishia kuwa inawezekana iwapo wataendelea kujituma.

“Nipo hapa kukutia moyo. Kwenye macho yako unaweza ukahisi kama haiwezekani, lakini niamini mimi inawezekana,” amesema Zuchu.

Related Articles

Back to top button