Zuchu amtaka Mama yake kupuuza mitandao

DAR ES SALAAM: Msanii maarufu wa Bongo Fleva, Zuhura Othman maarufu kama Zuchu, amemshauri mama yake mzazi, Malkia wa Taarab Khadija Kopa, kupuuza maneno yanayoenezwa mitandaoni kuhusu maisha na kazi yake.
Hivi karibuni, sauti inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inadaiwa kumhusisha Khadija Kopa akielezea kutoridhishwa na jinsi mwanaye anavyotendewa na lebo ya Wasafi, akitaka Zuchu aondoke kwenye lebo hiyo ikiwa ananyanyaswa.
Katika mahojiano, Zuchu alieleza kuwa mama yake alikerwa na maneno yanayoenezwa kwenye kurasa za udaku mitandaoni, lakini yeye mwenyewe hana tatizo lolote na yuko sawa.
Aliongeza kuwa amemwambia mama yake avumilie kutokana na umaarufu wake, kwani watu wengi wanamfuatilia sana.
Kwa upande wake, Khadija Kopa amekanusha uvumi wa kuwa na ugomvi na Mama Diamond (Sanura Kassim).
Amesema hana shida na mtu yeyote, na kwamba maneno ya uzushi yanayozunguka mitandaoni hayana msingi. Ameongeza kuwa watu wanachochea ugomvi usiokuwepo kati yake na Mama Diamond, na amewataka waache tabia hiyo.
Aidha, Khadija Kopa amesisitiza kuwa sauti inayosambaa mitandaoni haimhusu Mama Diamond, bali ilikuwa ni mazungumzo yake na mtangazaji mmoja aliyekuwa akimuuliza kuhusu mambo ya mwanaye, Zuchu.
Ameeleza kuwa amechoshwa na habari za uzushi kuhusu mtoto wake na kutoa onyo kwa wale wanaomkosesha amani Zuchu waache mara moja.
Hali hii inaonyesha jinsi mitandao ya kijamii inaweza kuchochea taarifa zisizo sahihi na kusababisha taharuki kwa wasanii na familia zao.