Mastaa

Gigy Money: Mume wangu akiongeza mke wa pili bora tuachane

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Gify Stanford ‘Gigy Money’, amesema hayupo tayari kuona mume wake akiongeza mke wa pili, akisisitiza kuwa hatua hiyo inaweza kuwa sababu ya kuvunjika kwa ndoa yao.

Gigy amesema licha ya kufahamu kuwa mume wake ni muislamu na dini inaruhusu kuoa zaidi ya mke mmoja, yeye binafsi hawezi kukubaliana na hali ya kugawana mume na mwanamke mwingine kutokana na tabia yake ya kuwa na wivu.

Gigy amesema anaamini yeye pekee anatosha katika ndoa yake na haoni sababu ya mume wake kutafuta mwanamke mwingine.

“Najua mume wangu ni Muislamu, lakini ikifika hatua ya kuongeza mke wa pili, hilo siwezi kulikubali. Mimi nina wivu na naamini ninatosha kama mke,” amesema Gigy.

Msanii huyo amehoji mantiki ya mwanaume kuwa na wake wawili huku akisisitiza kuwa wanawake wote wana hadhi sawa.

“Kwa nini mpenzi mmoja ashare watu wawili? Mimi ni mwanamke na huyo atakayemuoa pia ni mwanamke kama mimi. Sina tofauti naye, sasa huko anafuata nini?” amehoji.

Gigy ameongeza kuwa endapo mume wake atachukua uamuzi wa kuoa mke mwingine, yeye ataona ni bora kila mmoja aendelee na maisha yake badala ya kuendelea na ndoa yenye migogoro.

Katika mazungumzo hayo, Gigy pia amezungumza kuhusu ndoto yake ya kupata mtoto mwingine mapema, akieleza kuwa anatamani siku moja mtoto wake aje kuwa sehemu ya familia ya wasanii maarufu Zuchu na Diamond Platnumz kupitia ndoa.

Hata hivyo, amebainisha kuwa kupata mtoto si jambo jepesi kama wengi wanavyofikiri, kwani wanandoa hupitia changamoto mbalimbali katika safari ya uzazi.

“Watu wanafikiri kupata mtoto ni jambo rahisi, lakini si hivyo. Kupata mtoto mwingine kunahitaji maandalizi na wakati sahihi kwa sababu wanandoa hupitia mambo mengi katika maisha ya ndoa,” amesema.

Gigy Money amezua mijadala kwa mashabiki wake kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi wakimuunga mkono na wengine wakieleza kuwa suala la wake wengi linategemea makubaliano na imani za wahusika.

Related Articles

Back to top button