Waitara Trophy kutimua vumbi Jumamosi

DAR ES SALAAM: Shindano la Gofu la kumuenzi Mkuu wa Majeshi wa zamani Jenerali mstaafu George Waitara ‘NBC Waitara Trophy’ linatarajia kufanyika Jumamosi ya wiki hii kwenye Viwanja vya Gofu Lugalo Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Dar es Salaam Leo Mwenyekiti wa Klabu ya Gofu Brigedia Jenerali mstaafu Michael Luwongo amesema wanatarajia ushiriki mkubwa wa wachezaji kutoka klabu mbalimbali nchini.
Amesema anaamini shindano hilo litakuwa lenye ushindani mkubwa kwa kuwa litashirikisha wachezaji wakubwa na wenye uzoefu katika michuano mikubwa.
Waitara ni muasisi wa klabu ya Lugalo na ndiye muanzilishi wa Viwanja vya Gofu kwenye klabu hiyo hivyo wanamuenzi kutambua mchango wake katika michezo nchini.
“Nawashukuru benki ya NBC ambao kila mwaka wanadhamini shindano hili. Mwitikio wa washiriki ni mkubwa na tunategemea watakuwa wengi sana.
Washiriki ni wa madaraja yote kuanzia watoto, vijana, wanawake na wazee,”amesema.
Amesema washindi wote watapewa zawadi mbalimbali zilizoandaliwa kwa kila daraja katika hafla itakayofanyika siku hiyo jioni.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Masoko wa NBC David Raymond amesema wao kama wadau wakubwa wa michezo wana dhamira ya dhati ya kukuza mchezo huo.
Amesema huu ni msimu wa nne wamekuwa wakisapoti shindano hilo na kutoa wito kwa washiriki kujitokeza kwa wingi kuona shindano hilo na jinsi washindi watakavyokuwa wanakabidhiwa zawadi zao.
Nahodha wa Gofu Lugalo Meja Japhet Masai amesema droo ya shindano hilo kwa ajili ya kupanga timu na wachezaji itafanyika kesho Alhamis.