UEFA kuondoa tishio kususia mashindano ya Fifa

MONACO: Droo ya hatua ya ligi ya UEFA Champions League msimu huu imekumbwa na mvutano mkubwa kati ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kufuatia mpango wa kuingiza wawekezaji binafsi katika uendeshaji wa mashindano makubwa ya FIFA.
UEFA, ambayo ina vilabu na timu za taifa zenye mchango mkubwa katika uchumi wa soka duniani, ilikasirishwa baada ya kufichuka mwishoni mwa Julai kuwa FIFA, chini ya Rais Gianni Infantino, ilikuwa ikipanga kuanzisha kampuni ya kibiashara itakayohusika na kuendesha matukio makubwa kama Kombe la Dunia na Kombe la Dunia la Vilabu.
Mpango huo ungewezesha wawekezaji binafsi kununua hisa katika kampuni ambayo ingeundwa kupitia mpango wa FIFA Forward Enterprise (FFE).
Rais wa UEFA, Aleksander Čeferin, alikosoa vikali mpango huo na kuutaja kuwa ni mpango wa siri na usio wazi unaofanyika nyuma ya pazia.
UEFA pia ilitoa onyo kali kwamba timu za taifa za Ulaya zisingeshiriki mashindano yoyote ya FIFA endapo mpango huo ungeendelea.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa vyanzo vya AFP zinaeleza kuwa UEFA inatarajiwa kuondoa tishio hilo baada ya viongozi wa shirikisho hilo pamoja na vyama wanachama vya Ulaya kukutana Monaco siku ya Alhamisi, muda mfupi kabla ya droo ya Champions League.
UEFA ilikuwa imedai mpango huo uachwe kabisa, huku pia ikitaka kuhakikishiwa kuwa juhudi za kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa soka kwa namna hiyo hazitarudiwa tena.
Chanzo kimoja kiliiambia AFP kuwa UEFA imeridhishwa kwamba sharti hilo la pili sasa limetimizwa.
Hatua hiyo pia itaisaidia UEFA kuendelea kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu suala la kutaka Infantino aondoke katika nafasi yake, kwani kususia mashindano ya FIFA kungeweza kuvuruga umoja wa vyama vya Ulaya endapo baadhi yao vingekataa kushiriki.
Mashindano mbalimbali bado yanaendelea chini ya FIFA, ikiwemo Kombe la Dunia la Wanawake chini ya miaka 20. litakalofanyika Poland mwezi ujao, huku michuano ya kufuzu Kombe la Dunia la Wanawake 2027 nchini Brazil ikiendelea barani Ulaya.




