Ubora wa wachezaji uliamua mechi

DAR ES SALAAM: KAIMU Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Hemed Suleiman ‘Morocco’, amesema ubora wa wachezaji wa DR Congo uliamua matokeo ya mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).
Amesema wachezaji walicheza vizuri na kutengeneza nafasi lakini wamekosa nyota wenye ubora ambao wangeamua matokeo katika mchezo wa jana dhidi DR Congo, uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Stars ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya DR Congo katika mchezo huo wa kundi H na kuifanya Stars kushuka hadi nafasi ya tatu wakisalia na alama tatu huku Guinea wakichupa hadi nafasi ya pili baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Ethiopia.
“Tumepoteza mechi kwa sababu ya ubora wa wapinzani wetu, wachezaji wao waliamua mechi, sisi tulitengeneza nafasi tukashindwa kuzitumia,”amesema Morocco.
Amesema licha ya kufungwa haina maana ya kutofuzu kwa sababu kuna mechi mbili, jambo la msingi ni kusahau matokeo hayo na kujipanga kwa mechi ijayo,” amesema.
Morocco amesema wanarejea uwanja wa mazoezi kusahihisha makosa yaliyojitokeza ikiwemo suala la umakini wa washambuliaji kutumia nafasi wanazotengeneza kuwa mabao.
“Hatujakata tamaa nina imani ya kushinda michezo miwili iliyosalia dhidi ya Guinea na Ethiopia na kupata alama sita zitakazotupeleka kucheza fainali za AFCON,” amesema.