Tutaishangaza Nigeria leo – Nahodha Chebbak

RABAT: NAHODHA wa timu ya Wanawake ya Morocco, Ghizlane Chebbak ana imani kuwa Atlas Lionesses wanaweza kuishinda Nigeria katika fainali ya leo usiku Jumamosi ya Julai 26, 2025 ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake, licha ya kukabiliana na timu iliyofanikiwa zaidi barani afrika kwa sasa.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 34, ambaye amekuwa hazina kubwa ya Morocco katika kipindi chote cha michuano hiyo, atakuwa anacheza fainali yake ya pili mfululizo ya WAFCON baada ya huzuni ya kushindwa nyumbani na Afrika Kusini miaka mitatu iliyopita.
Kushindwa huko kunasalia kuwa kumbukumbu chungu kwa fowadi huyo mkongwe, Alisaidia sana Morocco kutinga fainali ya 2022 na amekuwa muhimu tena kwa mafanikio yao, kwani kwa sasa ni mfungaji bora akiwa na mabao manne licha ya kufifia kwa kiasi fulani katika hatua ya mtoano.
“Juhudi zetu zilitufikisha katika hatua hii na tunatamani sana kucheza fainali, haswa dhidi ya timu inayojulikana kama Nigeria,” amesema Ijumaa kwenye mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi.
“Tulicheza nao katika nusu fainali kwenye mashindano yaliyopita, na tunajua itakuwa timu kubwa na nzuri, na tutalazimika kushinda.”
Uzoefu wa mshambuliaji huyo utakuwa muhimu dhidi ya timu ya Nigeria ambayo imeshinda mataji tisa ya WAFCON na haijawahi kupoteza fainali. Chebbak alikuwa sehemu ya timu ya Morocco iliyoiondoa Nigeria kwa penalti 5-4 katika nusu-fainali ya 2022, mechi ambayo ilishuhudia Super Falcons wakipunguzwa hadi wachezaji tisa kufikia dakika ya 72.




