Kuogelea

TSA yatangaza kikosi mashindano ya Afrika Kanda ya 3

DAR ES SALAAM: CHAMA cha Kuogelea Tanzania (TSA) kimetangaza kikosi cha awali cha waogeleaji watakaoiwakilisha nchi katika Mashindano ya Africa Aquatics Kanda ya 3 yatakayofanyika Nairobi, Kenya kuanzia Oktoba 16 hadi 19 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Ufundi wa TSA, Amina Mfaume, kikosi hicho kimejumuisha vipaji vya waogeleaji kuanzia umri wa miaka 11 na kuendelea, hatua inayodhihirisha uwekezaji mkubwa katika kukuza mchezo huo nchini.

Katika hatua ya kuvutia zaidi, timu hiyo pia inatarajiwa kuwa na waogeleaji wakongwe (masters), jambo linaloonesha dhamira ya TSA kukuza mchezo huo kwa makundi yote ya umri.

Hata hivyo, orodha ya mwisho ya wateule hao bado inasubiri uthibitisho wa ushiriki kutoka kwa wazazi au walezi, na itawekwa wazi mara baada ya mchakato huo kukamilika ifikapo Julai 20, 2025.

“Ili kuhakikisha maandalizi ya kiwango cha juu, TSA imepanga kuanzisha kambi maalum ya mazoezi ya mchana kuanzia Agosti. Kambi hiyo itafanyika kwa mfumo wa kikanda na kuendeshwa na makocha wa kitaifa wakiongozwa na Kocha Mkuu wa Taifa, Alexander Mwaipasi.

Kocha Mwaipasi atashirikiana na Kocha Kanisi Mabena na Kocha Agness Kimimba kwa mazoezi ya waogeleaji wa Dar es Salaam. Kwa upande wa Kanda ya Ziwa, waogeleaji watafundishwa na Kocha Ally Msazi, huku waogeleaji wa Arusha wakishauriwa kuwasiliana na Kocha Fiete kwa ajili ya mipango ya kambi yao.

“Tunaamini timu hii si tu kwamba ina vipaji, bali pia ina ari ya kuiwakilisha nchi kwa heshima na mafanikio. Uwepo wa makocha wenye uzoefu unazidi kutupa matumaini ya kufanya vizuri Nairobi,” alisema Amina Mfaume.

TSA inatarajia mashindano haya kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kukuza mchezo wa kuogelea nchini na kutoa fursa kwa wanamichezo chipukizi kung’ara katika ngazi ya kimataifa.

 

Related Articles

Back to top button