Taylor Swift kusimamia shoo usiku wa Grammy kesho

LOS ANGELES: MWANAMUZIKI anayeongoza kwa mkwanja mrefu kuliko wanamuziki wote wa kike duniani, Taylor Swift ametangazwa kuwa mmoja wa watangazaji katika hafla ya Tuzo za Grammy zitakazofanyika kesho Jumapili ya Februari 2 huko Los Angeles nchini Marekani.
Taarifa kutoka ukurasa wa mtandao wa X wa waandaji wa tuzo hizo umeandika: Je, uko tayari kwa hilo? @taylorswift13 atajiunga nasi Jumapili hii kama mtangazaji kwenye GRAMMYs ya 67,” ilisema tarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kwamba Swift atapanda jukwaani kama mtangazaji na atakabidhi kombe la heshima kubwa zaidi katika muziki licha ya kutoweka wazi itakuwa ni kipengele gani mwanamuziki huyo atashiriki katika tukio hilo.
Licha ya Swift kutarajiwa kushiriki tukio hilo kama mtangazaji ikumbukwe kuwa naye ameteuliwa kuwania tuzo kwa usiku huo ambapo atawania tuzo ya albamu ya mwaka kupitia albamu yake ya “The Tortured Poets Department,” na tuzo nyingine tano.
Washindani wake wa tuzo hizo kwa usiku huo ni pamoja na Beyonce kupitia albamu yake ya “Cowboy Carter” na mwanamuziki Billie Eilish akiwa na albamu yake ya “Hit Me Hard and Soft.”
Onyesho la Grammys litasherehekea maonesho bora katika muziki na pia kuchangisha pesa kwa watu walioathiriwa na milipuko ya hivi karibuni katika jiji la Los Angeles.