TASIMA Wapiga Hodi BASATA

DAR ES SALAAM: Chama cha Muziki wa Singeli Tanzania (TASIMA) leo kimefanya ziara katika ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kikao maalum kilichoongozwa na Katibu Mtendaji wa BASATA, Dk Kedmon Mapana.
Ujumbe wa TASIMA umeongozwa na Mwenyekiti wao, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uswazi Born Talent inayojihusisha na ukuzaji wa Muziki wa Singeli, Bwana Massoud Kandoro, maarufu kama Kandoro Baba.
Kikao hicho kililenga kujadili mbinu bora za kukuza, kulinda, na kuendeleza Muziki wa Singeli nchini, pamoja na kuutangaza kimataifa kama alama muhimu ya utamaduni wa Tanzania.
Kandoro Baba alieleza changamoto za wasanii wa Singeli, ikiwemo ukosefu wa fursa, urasimishaji wa kazi zao, na ushirikiano wa karibu na wadau mbalimbali. Alisisitiza umuhimu wa kutoa msaada wa kisheria kwa wasanii ili kulinda haki zao za kiakili na kibiashara.
Kwa upande wake, Dk Mapana aliipongeza TASIMA kwa juhudi zake za kukuza sanaa ya Singeli na kuahidi kutoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha muziki wa Singeli unakua kwa viwango bora na unapata heshima inayostahili kitaifa na kimataifa. Alisisitiza kuwa BASATA itahakikisha kuwa wasanii wa Singeli wanapata nafasi ya kushirikiana na wadau mbalimbali na pia kusaidiwa katika masuala ya urasimishaji wa kazi zao.
Kikao hiki ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba muziki wa Singeli unaimarika na kuwa na mchango mkubwa katika utambulisho wa kitamaduni wa Tanzania, huku ukiendelea kuvutia hadhira mpya ndani na nje ya nchi.