Nyumbani

Tanzanite yaanza maandalizi ya Kombe la Dunia

DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 20, Tanzanite Queens, imeendelea na maandalizi kuelekea Fainali za Kombe la Dunia la Wanawake U20 zitakazofanyika nchini Poland Septemba mwaka huu, huku Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likipanga kambi ya kimataifa itakayohusisha mechi tatu za kirafiki.

Tanzanite Queens imeendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kambi ya ndani inayolenga kukiandaa kikosi hicho kabla ya kuelekea hatua ya maandalizi ya mwisho nje ya nchi.

Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Oscar Mirambo, amesema baada ya kambi ya ndani, timu hiyo itaweka kambi ya kimataifa kwa siku 14, ambapo itatumia muda huo kucheza michezo ya kirafiki kama sehemu ya maandalizi ya fainali hizo.

“Tunajiandaa na mashindano ya Kombe la Dunia ya Wanawake, tumeanza na kambi ya ndani na kimataifa tutaenda kwa siku 14. Ndani ya siku hizo tutacheza michezo ya kirafiki,” amesema Mirambo.

Mirambo amesema hadi sasa Marekani imekubali kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Tanzanite Queens, hatua ambayo amesema itakuwa muhimu kwa kikosi hicho kupata uzoefu na ladha ya ushindani wa kimataifa kabla ya kwenda Poland.

Mchezo huo wa kirafiki unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya Tanzanite Queens, kutokana na ubora na uzoefu wa Marekani katika soka la wanawake, huku kikosi hicho kikiendelea kujenga uwezo wa kukabiliana na timu zenye viwango tofauti katika Kombe la Dunia.

Ushiriki wa Tanzania katika fainali hizo za Kombe la Dunia U20 unatarajiwa kuwa fursa kubwa kwa wachezaji hao kuonesha vipaji vyao kwenye jukwaa la kimataifa na kuongeza uzoefu wa soka la kiwango cha juu.

Related Articles

Back to top button