T-Pain Auza Katalogi Yake ya Muziki kwa Mwekezaji

RAPA maarufu wa Hip-Hop na R&B kutoka Marekani, Faheem Rashad Najm, anayejulikana kama T-Pain, ameuza katalogi yake ya muziki pamoja na baadhi ya masters zake kwa mwekezaji kwa kiasi cha pesa ambacho hakijawekwa wazi.
Hatua hii inamfanya T-Pain kuwa miongoni mwa wasanii kadhaa wa kimataifa waliouza haki zao za muziki katika miaka ya hivi karibuni, wakitafuta faida kubwa kutokana na kazi zao.
Kwa mujibu wa United Masters, T-Pain alikuwa miongoni mwa wasanii wachache wa enzi yake walioweza kumiliki sehemu ya masters zao.
Hii ni kwa sababu wasanii wengi wa wakati huo walikuwa wakisainiwa mikataba na makampuni ya muziki yaliyowanyima umiliki wa kazi zao. Uamuzi wake wa kuuza katalogi yake ni hatua ya kibiashara ambayo inazidi kuwa maarufu katika sekta ya muziki duniani.
Hatua hii ni funzo kwa wasanii wa kizazi kipya kuhusu umuhimu wa kumiliki masters zao. Kwa kumiliki haki hizi, msanii anaweza kuzitumia kwa uhuru, iwe ni kwa faida ya baadaye au kuziuza kwa dau kubwa pale inapohitajika.
Kwa upande wa wasanii wa Bongo Fleva, swali linabaki: Kama sanaa yako ingekuwa na thamani ya mamilioni, ungeendelea kuimiliki au ungeiuza kwa dau kubwa?