Kwingineko

Stones achekelea unahodha England

MLINZI wa kati wa Manchester City John Stones atakuwa nahodha wa England dhidi ya Ugiriki uwanjani Wembley leo usiku, wakati ambao meneja wa muda wa timu hiyo Lee Carsley amefichua kuwa nahodha wake Harry Kane ataanzia kwenye benchi kutokana na kile alichokiita “kijeraha kidogo”.

Kane aliumia kwenye mechi ya mwisho ya Bayern Munich kabla ya mapumziko ya kimataifa na amefanya mazoezi pembeni na kundi kuu la wachezaji wa England siku mbili zilizopita walipokuwa wakijiandaa na mechi hiyo ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Stones kuwa nahodha wa timu hiyo akianza katika kikosi cha kwanza.

Akizungumzia suala hilo meneja wa muda wa timu hiyo Lee Carsley amesema Stones anastahili kuwa nahodha wa kikosi hicho akitaja sababu mbalimbali ikiwemo uzoefu.

“Harry anauguza jeraha dogo, kajigonga kidogo, jambo ambalo hatutatilia manani. Nimekuwa na mazungumzo mazuri na John nilimuomba awe nahodha wa timu. Ni kitu anachostahili kwa mechi alizocheza, uzoefu alionao, kiwango alichoonesha, amekuwa mfano wa kuigwa kwa wachezaji wetu chipukizi” amesema kocha Carsley

Stones ambaye ataiongoza timu hiyo kwenye mechi yake ya 82 ya timu ya taifa, amesema kuwa nahodha wa timu hiyo ni kila kitu alichohitaji katika maisha yake ya soka na ni heshima kuvaa kitambaa cha unahodha wa taifa hilo maarufu la soka duniani.

“Ni kitu ambacho nilitamani tangu nikiwa mtoto. Zaidi ni kwa familia yangu, kuniona nikiingia uwanjani kama nahodha wa England ni wakati muhimu na maalum sana kwangu. Mtu ambaye siwezi kumshukuru vya kutosha ni kocha Lee haya yote yanatokea kwa sababu yake. Kuingia uwanjani na kitambaa ni heshima kubwa na ni wakati ambao nitauthamini milele.” Amesema Stones

Related Articles

Back to top button