Sitacheza ‘scene’ za kubusu midomo

NAIROBI: MWANAMUZIKI wa Kenya Sanaipei Tande amefunguka kitu asichoweza kufanya katika kazi yake ya uigizaji hata apewe kitu gani cha thamani.
“Sitabusu kwenye midomo, sitacheza kuhamasisha ngono ikiwa ndivyo inavyotakiwa… Sitafanya majukumu ya ushoga licha ya kutoegemea upande wowote kuhusu hilo. Pia sitakaa uchi katika uigizaji wangu,” ameeleza Tande.
Tande ameendelea kueleza: “Utu wangu hauniruhusu kufanya mambo fulani. Baadhi ya watu wanaamini kuchukua majukumu kama haya ni muhimu kwa ukuaji wa kazi, lakini kwangu, hiyo itakuwa kuvuka mipaka,”
Akizungumza katika mahojiano na Buzz Central, Tande amesema baadhi ya watu huwa na tabia ya kuwahusisha waigizaji na wahusika wao luningani, bila kujua kunaweza kuathiri katika maisha halisi.
Ameongeza kuwa, wakati uigizaji unahusu kujumuisha majukumu tofauti, watazamaji wengine wanazama sana katika tabia inayoonyeshwa na muigizaji na kusababisha fikra zisizofaa.
Kwa sasa Tande ni sehemu ya waigizaji wa Kash Money, ambapo anacheza nafasi ya mke wa Sosholaiti. Akiongea katika mahojiano ya awali na TUKO, ameeleza kuwa changamoto ya kucheza mhusika ambaye anazungumza Kiingereza kabisa ilimvutia sana kwa kuwa ndiyo lugha yake mama.
“Nilivutiwa na jukumu hilo kwa sababu sikuwahi kucheza mke wa Sosholaiti hapo awali. Ilikuwa pia changamoto kwa kuwa maonesho mengi ambayo nimefanya yalikuwa mchanganyiko wa Kiingereza na Kiswahili. Kuzungumza Kiingereza safi kulichukua muda wa kuzoea. Zaidi ya hayo, kufanya kazi pamoja na waigizaji ambao nimewajua kwa miaka mingi kulirahisisha kazi yangu na kuongeza umakini mno,” amesema.