Siri ya mabao ya Buba iko kwa Mama yake

DAR ES SALAAM: WINGA mpya wa Yanga Buba Jammeh amesema alitabiri kufunga katika mchezo wake wa kwanza baada ya kuzungumza na mama yake kabla ya mechi, aliyempa ushuri uliomtia nguvu ya kuifungia timu yake mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Cosmopolitan ya First League uliochezwa jana kwenye Uwanja wa KMC.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Buba amesema kabla ya kushuka dimbani alipiga simu nyumbani na kumuomba mama yake amuombee ili afunge katika mechi hiyo ya kwanza, jambo ambalo lilitimia na kumpa furaha kubwa.
Nyota huyo alieleza kuwa ingawa ameanza kwa kufunga mabao mawili, bado hajaonesha kiwango chake halisi kutokana na kuwa ndiyo kwanza ameanza kucheza katika ligi mpya, akiahidi kuwa kadri muda unavyokwenda ataendelea kuimarika.
Ameongeza kuwa mchezo huo ulikuwa mzuri kwake kwa kuwa ulikuwa ni wa kwanza akiwa na kikosi cha Yanga, huku akiamini mechi zijazo zitakuwa bora zaidi baada ya kuzoea mfumo wa timu na ushindani wa ligi.
Winga huyo mpya aliwashukuru mashabiki wa Yanga kwa mapokezi makubwa waliyompa baada ya mchezo huo, akisema hajawahi kushuhudia hali kama hiyo ambapo mashabiki walimpongeza na kumpa zawadi ya fedha, jambo lililompa hamasa ya kufanya vizuri zaidi.
Nyota huyo wa Gambia ni ingizo jipya kupitia dirisha dogo la usajili hivi karibuni.
Mwisho




