Simba Yawinda Ushindi dhidi ya Al Masry leo

MISRI:KIKOSI cha Simba SC, kinachonolewa na Kocha Fadlu Davids, kitashuka dimbani leo katika mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry. Mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Suez, nchini Misri.
Simba itaanza ugenini kwenye mchezo huu wa kwanza, huku marudiano yakitarajiwa kufanyika Aprili 9 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam. Mshindi wa jumla katika michezo hii miwili atafuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kocha Fadlu Davids amesema kuwa kikosi chake kimefanya maandalizi ya kutosha wakati wa kambi yao huko Ismailia, Misri, na wachezaji wako tayari kwa pambano hili muhimu.
“Tumekuwa na maandalizi mazuri kwa siku zote tulizokuwa Ismailia. Jana tumefanya mazoezi ya mwisho hapa Suez. Tunakutana na timu yenye ubora wa juu, inayoshika nafasi ya nne kwenye ligi ya Misri, jambo linaloashiria ushindani mkubwa,” amesema Davids.
Kocha huyo pia ameeleza kuwa wamefanya uchambuzi wa kina kuhusu Al Masry na kubaini wachezaji watatu hatari kwenye safu yao ya ushambuliaji.
“Tunaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa, huku tukilenga kupata matokeo mazuri ugenini. Tunajua ubora wa wapinzani wetu, lakini hatutacheza kwa kujiamini kupita kiasi. Tunahitaji kuwa makini na kutumia kila nafasi tunayopata,” ameongeza.
Mchezo huu ni muhimu kwa Simba, kwani matokeo mazuri ugenini yatawaweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu nusu fainali watakapocheza mchezo wa marudiano nyumbani.