Ni wakati Twiga Stars kuandika historia WAFCON
TIMU 12 zitashiriki fainali za soka za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon) zitakazofanyika Morocco mwakani.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo bendera yake itapepea Morocco wakati timu ya soka ya wanawake ya taifa, ‘Twiga Stars’ ikishiriki kwa mara ya pili michuano hiyo.
Twiga Stars imefuzu kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya ushindi wa nyumbani wa mabao 3-0 Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kabla ya kufungwa mabao 2-0 na Togo Uwanja wa Kegue, Lome.
Kabla ya kukutana na Togo, Twiga Stars iliitupa nje Ivory Coast kwa mikwaju ya penalti 4-2, baada ya sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 180. Tanzania imeandika historia ya kufuzu kwa mara ya pili baada ya kufuzu mara ya kwanza mwaka 2010 ikiwa imepita miaka 13 tangu ilipocheza fainali za Afrika Kusini.
Tanzania ndio nchi pekee ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati iliyofuzu baada ya Kenya na Burundi kushindwa kufuzu ambapo ilitolewa na Algeria kwa jumla ya mabao 6-1 na Kenya ikifungwa na Botswana kwa jumla ya mabao 2-1.
Uganda na Kenya zimewahi kufuzu hapo awali mara moja, Uganda ikishiriki kwenye fainali 2000 na kuishia hatua ya makundi. Kenya ilipata nafasi hiyo mwaka 2016 kwenye fainali
zilizofanyika Cameroon wakiwa Kundi B na kumaliza nafasi ya mwisho baada ya kushindwa kukusanya hata pointi moja.
Safari hii Watanzania watapenda kuona Twiga Stars ikicheza ama robo fainali au nusu na ikiwezekana fainali kwa sababu mwaka 2010 waliishia hatua ya makundi.
Kocha msaidizi wa sasa wa Twiga Stars, Ester Chabruma ndiye alikuwa mchezaji bora kwenye kikosi cha 2010 akiwa chini ya nahodha Sofia Mwasikili ambao wote kwa pamoja walifunga bao moja moja kwenye mashindano hayo sambamba na Fatma Swalehe.
Twiga Stars ilikuwa Kundi A na ilipoteza mechi zote tatu dhidi ya Nigeria, Afrika Kusini na Mali, ikifunga mabao matatu na kufungwa mabao nane.
Miaka 13 baadaye wanafuzu licha ya Ligi Kuu ya Wanawake kuanza kuchezwa nchini Tanzania miaka nane iliyopita, lakini pia Twiga Stars ina wachezaji wanaocheza kwenye klabu za nje ya nchi kama Opah Clement anayecheza Besiktasi ya Uturuki.
Aisha Masaka anayechezea klabu ya BK Häcken, Juliet Singano anayekipiga FC Juarez ya nchini Mexico bila kumsahau Enekia Kasonga anayekipiga Eastern Flames ya Saudi Arabia.
Uwepo wa wachezaji wanaocheza kwenye ligi zenye ushindani mkubwa kumesaidia kiasi kikubwa mafanikio ya Twiga Stars ambayo yalikuwa yakisubiriwa kwa maika 13. Pia ushindani mkubwa wa ligi ya wanawake nchini umechangia kuzalisha vipaji vingi vilivyosaidia kuiinua Twiga Stars.
Klabu za nyumbani zimeleta ushindani mkubwa kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kutoa mara mbili timu kutoka ukanda huu kushiriki fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake tangu ilipoanzishwa mwaka 2021 ambazo ni Vihiga Queens (Kenya), Simba Queens na JKT Queens (Tanzania).
Katika miaka 13 iliyopita ligi ya wanawake ilikuwa haichezwi hali iliyochangia Twiga Stars iliyofuzu wakati huo kutokushinda hata mchezo mmoja kwenye Kundi A.
Lakini mazingira ya sasa ya upatikanaji wa wachezaji na pia ushindani wanaopata ndani na nje katika Ligi Kuu na mashindano mengine kunaiongezea Twiga Stars uwezekano wa kufanya vema zaidi katika Wafcon ya 2024 huko Morocco kuliko ilivyokuwa mwaka 2010 huko Afrika Kusini.
Pengine michuano hii itakuwa ya kwanza kwa timu za Ukanda wa Afrika Mashariki kufika hatua za juu zaidi lakini kufikia hatua hiyo ya kufuzu katika hatua ya mtoano bila shaka itawapasa Twiga Stars kupambana vilivyo ili kuzipiga vikumbo timu za nchi zenye uzoefu mkubwa na ambazo zimewahi kufaidi utamu wa mafanikio kama vile Nigeria, Afrika Kusini na Ghana.
Na kwa hakika wakati wa matayarisho ni sasa ili kudhihirisha azma hiyo. Mataifa hayo ni mabingwa wa kihistoria mara 11, Nigeria wakiwa wametwaa taji hilo katika fainali za 1991, 1995, 1998, 2000, 2002, 2004, 2006, 2010, 2014, 2016 na 2018, wenyeji Morocco, mabingwa watetezi Afrika Kusini wakitarajiwa kuwa moto zaidi, mabingwa mara tatu Ghana ambao wamerejea baada ya kukosekana kwa miaka sita, Algeria, Tunisia na Mali.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo walishiriki mwisho mwaka 2012,
Senegal, Zambia, Tanzania na Botswana yakikamilisha orodha ya timu zilizofuzu na
matarajio yanaelekezwa katika droo ambayo itatangazwa baadaye.
Mechi ya mwisho ya fainali ya Wafcon kati ya Morocco na Afrika Kusini iliweka rekodi ya mahudhurio ya mashabiki 50,000 waliohudhuria. Mechi hiyo ilitangazwa moja kwa moja katika maeneo zaidi ya 45, kwenye CAFTV na CAFOnline.com.
Mashindano yajayo ambayo yataandaliwa na taifa la Morocco wanaahidi kuwa tukio la
kusisimua na timu zenye tamaa ya ubingwa na wachezaji mashuhuri watashindana kuwania kombe.
Afrika Kusini inarudi kutafuta kuiga mafanikio yao ya kutetea taji la mwaka 2022 ambayo ilionesha kuboresha kiwango chake. Banyana Banyana walionesha ujasiri wakati Linda Mothlalo na Nicole Michael walipopata ushindi wa 2-0 dhidi ya Burkina Faso katika mechi ya marudiano katika Uwanja wa Lucas Moripe mjini Pretoria.
Algeria ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Burundi likifungwa na Ines Boutaleb na hivyo kufuzu baada ya kukosa mwaka 2022. Washindi wa medali ya shaba wa mwaka 1998, DRC walipata nafasi kwa ushindi wa jumla wa 3-2 dhidi ya Equatorial Guinea kufuatia sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza.
Botswana ilifuzu kwa kuifunga Kenya bao 1-0 katika Uwanja wa Taifa wa Botswana na kusonga mbele kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza.
Nigeria na Zambia zilifuzu kwa jumla ya mabao mengi na kukamilisha timu 12 itakazocheza katika mashindano hayo yatakayofanyika mwakani.
Baada ya kuchukua haki za kuwa mwenyeji, Morocco inatarajia kuchukua taji lao la kwanza
la Wafcon wakati ikishiriki kwa mara ya tano na kukuza soka la wanawake. Tunisia ilijikatia tiketi licha ya sare ya 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Congo na kushinda kwa jumla ya mabao 6-3 kwani mchezo wa awali walitoka 5-2.
Mashindano haya ambayo yalianzishwa mwaka 1991, hufanyika kila baada ya miaka miwili
na jumla ya mataifa 12 yatafuzu Wafcon na toleo moja katika kila miaka minne hutumika kutafuta kufuzu kwa Kombe la Dunia la Wanawake la Fifa Mungu ibariki Twiga Stars,
Mungu ibariki Tanzania.