Simba Marathon kusaidia wachezaji wa zamani

DAR ES SALAAM: MENEJA Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema fedha zitakazopatikana kupitia Simba Marathon zitakazofanyika Oktoba 4 zitatumika kuwasaidia wachezaji wa zamani wa klabu hiyo wanaokabiliwa na changamoto za kiafya na wanaohitaji matibabu.
Akizungumza Dar es Salaam Ahmed amesema hatua hiyo ni sehemu ya lengo la marathon hiyo, ambayo pamoja na kuhamasisha michezo na kuwaunganisha mashabiki, inalenga pia kugusa maisha ya waliowahi kuitumikia Simba.
“Tunakwenda kugusa maisha ya Wanasimba wenzetu ambao wametumikia Simba miaka huko nyuma, ambao kwa sasa wanahitaji msaada, hasa katika suala la matibabu na changamoto za kiafya,” amesema Ahmed.
Amesema Simba Marathon itakuwa na mbio za kilomita 21, kilomita 10 na kilomita tano za Fun Run, huku ikilenga kuwashirikisha mashabiki wa Simba, wapenzi wa riadha na michezo kwa ujumla.
Ahmed amesema baada ya mbio hizo, shughuli zitaendelea Coco Beach kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi usiku wa manane, zikihusisha burudani, vyakula, nyama choma, vinywaji pamoja na michezo ya watoto.
Amesema tukio hilo pia linakusudia kuwaunganisha mashabiki wa Simba katika mazingira ya kijamii na michezo, huku akiwataka watu mbalimbali kujisajili na kushiriki.
“Uwe shabiki wa Simba, uwe shabiki wa Namungo, shabiki wa Lipuli au hata kama huna timu, wote mnakaribishwa kushiriki Simba Marathon,” amesema.
Ahmed amewahimiza mashabiki na wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi Oktoba 4, akisema ushiriki wao utasaidia kufanikisha malengo ya tukio hilo, ikiwamo kuwafikia wachezaji wa zamani wanaohitaji msaada.




