Sheria mpya ya maktaba kupanua wigo wa maarifa

DAR ES SALAAM: HUDUMA za maktaba nchini zinatarajiwa kuimarika na kuwafikia wananchi wengi zaidi kufuatia maboresho ya Sheria ya Huduma za Maktaba Tanzania Na. 102 ya mwaka 2026, yanayolenga kuboresha uendeshaji wa maktaba na kuendana na mahitaji ya jamii katika zama za kidijitali.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, amewataka wakutubi na watunza nyaraka nchini kushiriki kikamilifu kikao kazi kitakachoitishwa hivi karibuni kwa ajili ya kujadili kanuni zitakazowezesha utekelezaji wa sheria hiyo.
Akizungumza katika hitimisho la Kongamano la Nne la Kimataifa la Huduma za Maktaba, Tamasha la Vitabu na Usomaji, pamoja na uzinduzi wa Mfumo Jumuishi wa Maktaba Mtandao wa Taifa (INDLS), jijini Dar es Salaam, Ruzegea amesema ushiriki wa wadau ni muhimu ili kuhakikisha kanuni zitakazotungwa zinazingatia mahitaji halisi ya watumiaji wa huduma hizo.
Amesema maboresho ya sheria hiyo yanalenga kupanua wigo wa huduma za maktaba na kuhakikisha wananchi ndani na nje ya nchi wanapata fursa zaidi za kujifunza na kupata maarifa.
“Ninatoa wito kwa wakutubi wote nchini na watunza kumbukumbu kujitokeza kushiriki kikao kazi tutakachoitisha hivi karibuni, kitakachojadili maeneo mbalimbali yanayohusu kanuni za uendeshaji wa Sheria Na. 102 ya mwaka 2026,” amesema Ruzegea.
Ameeleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha uelewa wa sheria na kuweka msingi wa kisasa wa utoaji huduma za maktaba, sambamba na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, amesema kongamano hilo limefanikiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya taaluma ya ukutubi, matumizi ya teknolojia na namna ya kuimarisha utamaduni wa kusoma nchini.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa ni matumizi ya akili unde (AI) katika huduma za maktaba, maboresho ya mitaala ya ukutubi na sayansi ya taarifa, pamoja na dhana ya embedded librarianship inayolenga kuwafikisha wakutubi na huduma zao karibu zaidi na watumiaji.
Kwa upande wake, Profesa Evans Mwema wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema ni muhimu matumizi ya AI yajumuishwe katika mitaala ya ukutubi ili kuwajengea wataalamu uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi wa kazi, kuimarisha upatikanaji wa taarifa na kukuza usomaji katika jamii.
Kongamano hilo pia lilijadili namna ya kuimarisha Chuo cha SLADS ili kuboresha mafunzo ya wataalamu wa maktaba na sayansi ya taarifa, pamoja na masuala ya uwajibikaji, mapambano dhidi ya rushwa na taratibu za manunuzi ya umma.
Ruzegea amewahimiza wananchi, hususan vijana, kutumia maktaba kama vituo vya kujifunza, kubadilishana mawazo na kukuza vipaji, akisisitiza kuwa maktaba hazipaswi kuonekana kama maeneo ya kusoma vitabu pekee.
Amesema ushirikiano na wadau wa sanaa unaweza kuongeza mvuto wa maktaba kupitia shughuli za muziki, ngoma na michezo ya kielimu, hivyo kuwavutia watu wengi zaidi katika utamaduni wa kusoma.
Amewashukuru washiriki na taasisi mbalimbali zilizoshiriki kongamano hilo, akisema maazimio yake yatachangia kuimarisha huduma za maktaba na kuziandaa kukidhi mahitaji ya wananchi katika miaka ijayo.




