Sh bilioni 1.2 za mirabaha kugawanywa kwa wasanii

DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema katika kipindi cha Septemba 2023 hadi Novemba 2024 Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya jumla ya sh bilioni 1.2 za mirabaha ambazo zitagawanywa kwa wasanii.
Akitoa taarifa hizo Dar es Salaam leo Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma ‘Mwanafa’ amesema kati ya fedha hizo asilimia 70 zitaganywa kwa wasanii, asilimia 20 zitaingia Cosota na asilimia 10 zitaingia mfuko mkuu wa serikali.
Amesema baada ya makato mengine ya serikali, katika sh milioni 836.8 zitatolewa sh milioni 119.5 zitaingizwa kwenye mfuko wa utamaduni na sanaa zitakazobaki sh milioni 717.3 zitagawanywa kwa wasanii.
“Hakika haya ni mabadiliko makubwa katika sekta ya hakimiliki shukrani za kipekee zimfikie Rais kwa kuridhia mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na kuanzisha chanzo hiki cha tozo ya hakimiliki,”amesema.
Amesema kumekuwa na chachu ya mapato kuongezeka ikizingatiwa kuwa mgao uliofanywa na COSOTA Julai 2023 kwa kazi za muziki ulikuwa ni Shilingi milioni 396.9 na jumla ya wanufaika 8,018.
Amesema chanzo hiko kipya kimekusanya mapato zaidi na kitanufaisha wasanii na waandishi wa kada zote ukilinganisha na fedha iliyogawiwa kwa wasanii walionufaika mwaka 2023 katika mgao wa mwisho.
Mwinjuma amesema mirabaha hiyo inategemewa kugawiwa haraka punde tu baada ya fedha hizo kupokelewa kutoka Wizara ya Fedha.