Serengeti, Ngorongoro zawajua wapinzani Afcon

CAIRO:TIMU za Taifa za vijana za mpira wa miguu chini ya umri wa miaka 17 na 20 zimewajua wapinzani wao katika droo iliyochezeshwa Leo Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) jijini Cairo, Misri.
Katika mashindano ya AFCON U17 ambayo yatafanyika nchini Morocco mwaka huu yatashirikisha timu 16 ambazo zimepangwa katika makundi manne yenye timu nne kila moja.
Timu ya Taifa ya U17 ‘ Serengeti Boys’ inayoshiriki mashindano hayo kwa mara ya tatu imepangwa Kundi A pamoja na wenyeji Morocco, Uganda na Zambia.
Kundi B lina timu za Burkina Faso, Afrika Kusini, Misri na timu nyingine kutoka UNIFFAC na moja itakayojulikana baadaye.
Bingwa mtetezi Senegal yupo kundi C pamoja na Gambia, Somalia na Tunisia na Kundi D lina timu za Mali, Angola, Ivory Coast na timu nyingine kutoka Uniffac mbili zitajulikana baadaye.
Kwa upande ya timu ya U20 maarufu kama Ngorongoro Heroes imepangwa kundi A na wenyeji Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Ghana.
Kundi B lina timu za Nigeria, Misri, Afrika Kusini na Morocco na Kundi C lina timu za Senegal, Zambia, Kenya na Sierra Leone.
Kwa upande wa futsal AFCON kwa wanawake itakayofanyika Morocco baadaye mwaka huu timu ya wanawake imepangwa Kundi C pamoja na Madagascar na Senegal.
Kundi A lina timu za Morocco, Cameroon na Namibia na Kundi B lina timu za Angola , Misri na Guinea.