Simba kamili gado kuwavaa Cs Sfaxien

DAR ES SALAAM: NI habari njema kwa mashabiki wa Simba, baada ya beki Abdulrazack Hamza na kipa, Aishi Manula kurejea uwanjani.
Abdulrazack alipata majeraha kwenye mchezo wa hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine na kusababisha kutomaliza mechi.
Manula alishindwa kusafiri na timu kwenda Algeria kwa sababu ya changamoto ya kiafya, sasa amerejea kikosini kuendelea na maandalizi ya mchezo wa tatu wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ua Cs Sfaxien Jumapili, Desemba 15, Uwanja wa Benjamini Mkapa.
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema maandalizi kuelekea kwenye mchezo huo yanaendelea vizuri na wachezaji Abdulrazack na Manula wamerejea uwanjani tayari kuwavaa Cs Sfaxien.
“Ni habari njema kurejea wa beki wetu Abdulrazack na Manula tunayarajia kuwapa furaha mashabiki na wanasimba wote kwa sababu ya maandalizi mazuri yanayoendelea kufanyika chini ya kocha wetu, Fadlu Davids.
Kampeni yetu ya kutafuata alama tatu za nyumbani kwa kila mechi inaendelea na Jumapili, tunaenda kukusanya alama zetu zingine tatu,” amesema.
Ahmed amesema kila timu kati ya nne zilizopo kwenye kundi lazima zitoe pointi tatu, CS Sfaxien watatoa pointi tatu kwa Simba.