Rotimi, Vanessa penzi la mwendokasi

MUIGIZAJI na mwanamuziki maarufu kutoka Marekani, Rotimi, ambaye ni mume wa staa wa muziki wa Tanzania Vanessa Mdee ‘V Money’, amewahakikishia Watanzania kuwa ndoa yake na mkewe ipo imara na hawana mpango wowote wa kuachana.
Rotimi ametoa kauli hiyo kufuatia maneno mengi yaliyoenea mitandaoni baada ya yeye kuonekana akigawa namba yake ya simu kwa mwanamuziki mmoja wa kike anayeitwa Ronisia huko Paris, jambo lililoibua minong’ono na hisia tofauti miongoni mwa mashabiki.
Akizungumza kupitia video kwa msisitizo, Rotimi amefafanua wazi kuwa Vanessa Mdee ndiye mke wake wa pekee na hakuna jambo lolote linaloweza kuvunja ndoa yao.
“Aah Watanzania, hatuachani kamweeee, huyu ni mke wangu pekee,” amesema Rotimi huku akisisitiza mapenzi na heshima aliyonayo kwa mke wake.
Huku Vanesa akisisitiza kuwa hawaachani kamwe.
Kwa upande mwingine, mashabiki wamefurahishwa pia kuona juhudi za Vanessa Mdee katika kumfundisha mume wake lugha ya Kiswahili zikianza kuzaa matunda.
Rotimi ameonekana akizungumza maneno kadhaa ya Kiswahili, jambo ambalo pia amekuwa akilifanya kwa watoto wao, hatua inayozidi kuwavutia mashabiki wa wanandoa hao.
Kauli ya Rotimi imeonekana kuzima tetesi hizo na kurejesha matumaini kwa mashabiki waliokuwa na wasiwasi juu ya mahusiano ya wawili hao maarufu.




