Rihanna kuja na albamu ya 9

WASWAHILI husema subira yavuta heri! Baada ya mashabiki kusubiri kwa miaka mingi kwa hamu na shauku, hatimaye msanii na mwanamitindo maarufu kutoka Marekani, Robyn Rihanna Fenty, amethibitisha kuwa albamu yake ya tisa ipo njiani.
Rihanna, ambaye amejipatia umaarufu kupitia muziki na biashara zake, alifichua taarifa hiyo katika mahojiano na Harper’s Bazaar.
Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 37 alijulikana zaidi kupitia wimbo wake wa kwanza, “Pon de Replay,” alioutoa akiwa na umri wa miaka 17. Albamu yake ya mwisho, Anti, ilitoka mwaka 2016, lakini tangu wakati huo amejikita zaidi katika biashara, ikiwemo Fenty Beauty na Savage x Fenty.
Katika mahojiano hayo, Rihanna alisema alikuwa akitafuta mwelekeo sahihi wa kazi yake mpya. Alikiri kusikiliza tena albamu yake ya Anti ili kujua ni wapi anataka kuelekea na albamu hii inayokuja.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa hataki kutoa muziki usiolingana na ukuaji wake wa kisanii. “Siwezi kutoa kitu cha kawaida,” alisema Rihanna.
Kumekuwepo na uvumi kwamba albamu yake mpya ingekuwa na ladha ya reggae, lakini Rihanna alikanusha na kusisitiza kuwa kwa sasa hana mipaka yoyote ya aina ya muziki anaotengeneza.
Aliongeza kuwa licha ya kuwa mbali na muziki kwa muda, amekuwa akijitahidi kuhakikisha albamu yake mpya inakuwa na maana kubwa kwa mashabiki wake.
Rihanna pia alizungumzia changamoto za safari yake ya muziki na hofu aliyokuwa nayo hasa mwanzoni mwa taaluma yake. Licha ya changamoto hizo, ameendelea kuwa mmoja wa wasanii wa kike waliouza zaidi katika karne hii, huku mafanikio yake yakionekana pia kupitia biashara zake mbalimbali.
Akiwa sasa ni mama wa watoto wawili, Rihanna alisema kuwa uzazi umempa mtazamo mpya wa maisha na kazi yake.
“Najua muziki wangu mpya hautakuwa wa kawaida au wa kibiashara, lakini utakua mahali ambapo ubunifu wangu unastahili kuwa sasa,” alisema.
Kwa sasa, mashabiki wake wanasubiri kwa hamu uzinduzi wa albamu hii. Je, wewe ni mmoja wao?