Queen Darling atimiza miaka 40, mumewe ashindwa kujizuia

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Queen Darleen amesherehekea kutimiza umri wa miaka 40, huku mume wake, Isihack, akitumia siku hiyo maalumu kumwandikia ujumbe wa hisia uliojaa upendo, shukrani na faraja.
Katika ujumbe wake wa kumtakia heri ya kuzaliwa, Isihack ameeleza namna Queen Darleen alivyo mtu muhimu katika maisha yake, akimtaja kuwa mke na rafiki mwenye upendo mkubwa ambaye amekuwa naye katika nyakati mbalimbali za maisha, zikiwemo changamoto.
Amesema pamoja na kuwa na maneno mengi moyoni mwake, jambo analolihakikisha ni upendo mkubwa alionao kwa mwanamuziki huyo.
“Maneno mengi ninayo moyoni, lakini najua hakika kwamba nakupenda sana; wewe ni mtu muhimu sana katika maisha yangu. Umekuwa mke na rafiki mwenye upendo mwingi bila kujali changamoto zozote za maisha yetu,” ameandika Isihack.
Aidha, amegusia changamoto wanazopitia katika maisha yao, akimtakia mkewe nguvu na uvumilivu ili waendelee kuzivuka kwa msaada wa Mwenyezi Mungu.
Katika sehemu nyingine ya ujumbe huo, Isihack amemsifu Queen Darleen kwa kuwa mama bora wa familia, mwenye hekima na misingi imara.
Pia amemtia moyo asikate tamaa kutokana na hali mbalimbali za maisha, akisisitiza kuwa baada ya dhiki huja faraja.
Amehitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza umuhimu wa kudumisha maneno mawili katika maisha yao ya kila siku, ambayo ni “samahani” na “asante”.
Ujumbe huo umeifanya siku ya kutimiza miaka 40 ya Queen Darleen kuwa ya kipekee, huku ukionesha namna Isihack anavyothamini nafasi yake kama mke, rafiki na mama wa familia.




