Pedro: Yanga haibadilishi falsafa

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Pedro Goncalves, amesema licha ya safari ndefu kutoka Algeria, kikosi chake kipo tayari kurejea kwenye ushindani wa Ligi Kuu na kuendeleza kasi ya ushindi ambayo imekuwa utambulisho wa klabu hiyo.
Yanga inatarajia kumenyana na Namungo kesho katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania bara kwenye Uwanja wa KMC Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam leo kuelekea mchezo huo, Goncalves alisema maandalizi yamekuwa mafupi kutokana na ratiba ngumu ya safari, lakini falsafa na malengo ya Yanga hayajabadilika.
“Baada ya kurejea Algeria hatujapata muda mrefu sana wa kujiandaa. Safari ilikuwa ndefu. Changamoto yetu ni kuhakikisha hatutoki nje ya mstari wa malengo yetu. Sifa kubwa ya Yanga ni kushinda kila mechi, haijalishi mashindano gani,” alisema.
Kocha huyo alisema wanafanya kazi kwa bidii kurekebisha dosari walizoziona kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa na kwamba wanaiheshimu kila timu watakayokutana nayo.
“Tutacheza kama tunavyocheza mechi za Ligi ya Mabingwa. Falsafa yetu haitabadilika. Dhamira ni ushindi tu,” alisisitiza.
Goncalves alikiri kuwepo kwa baadhi ya majeraha ndani ya kikosi, lakini akasema hali inaendelea kuwa nzuri na anatarajia kuwa na asilimia kubwa ya wachezaji muhimu.
Kwa upande wake kipa wa Yanga Khomein Abubakar amesema safu ya timu imehamishia nguvu na malengo kwenye ligi ya nyumbani baada ya kumaliza ratiba ya Ligi ya Mabingwa.
“Tumemalizana na mechi za Ligi ya Mabingwa. Akili yetu sasa ipo nyumbani. Tupo imara kimwili na kiakili, na tupo tayari kupigania alama tatu muhimu,” alisema Khomein.
Ameitumia nafasi hiyo kuwaalika mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa KMC.




