Kwingineko

Pedro Rodriguez rasmi astaafu kucheza soka

BARCELONA: MSHAMBULIAJI wa zamani wa Barcelona, ​​Pedro Rodriguez, ametangaza rasmi kustaafu kucheza soka leo Jumatano, akieleza fahari yake kubwa ya kulitumikia soka.

Pedro, 39 katika shukrani zake kupitia ujumbe aliouandika kwenye Mtandao wa X, amezishukuru klabu, mashabiki na wachezaji wenzake alioshiriki nao katika safari yake hiyo ya takriban miaka 20.

“Nahisi wakati umefika. Ni wakati wa kupiga hatua mbele na kuanza sura mpya katika maisha yangu. Ninaondoka nikiwa na fahari ya kutimiza ndoto yangu, na fahari kwa kila mtu aliyeniunga mkono. Asante soka kwa kunipa furaha kubwa kiasi hiki.”

Mkongwe huyo anaondoka akiacha alama kama miongoni wa waliobeba karibu kila kombe aliloshiriki kuanzia ngazi ya klabu mpaka timu ya taifa, Uhispania.

Pedro alishinda ‘treble’ na mataji sita kwa mpigo (sextuple) akiwa na Barcelona, ​​klabu iliyomlea kupitia chuo chake cha vijana mpaka kufikia kilele cha uwezo wake aking’aa chini ya kocha Pep Guardiola.

Akiwa na Uhispania, alikuwa miongoni mwa nyota bora wa kizazi cha dhahabu, akiisaidia kutwaa Kombe la Dunia mwaka 2010 na Euro 2012, na hivyo kujiunga na orodha ya kipekee ya wachezaji walioshinda mataji yote makubwa.

Mbali na Barcelona, ​​Pedro pia aliacha alama yake kwa kutwaa Premier League akiwa na Chelsea kabla ya kuhamia Serie A alikojiunga na AS Roma kabla ya kutimkia Lazio.

Kwa ujumla, Pedro ametwaa UEFA Champions League mara tatu, Europa League mara moja, UEFA Super Cup mara moja, Kombe la Dunia la Klabu mara tatu, La Liga mara tano, Copa del Rey mara tatu, FA Cup mara moja na Supercopa de Espana mara nne.

Related Articles

Back to top button