Ligi Kuu

Pacome: Hatuna muda wa kupoteza, lengo alama tatu

DAR ES SALAAM: KIUNGO wa Yanga, Pacome Zouzoua, amesema kuwa kikosi chao hakina muda wa kupoteza kwani kila mchezo ni muhimu katika mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Yanga, ambao ni vinara wa ligi kwa sasa, wanajiandaa kwa mchezo wao ujao wa Kariakoo Derby dhidi ya Simba, mechi ambayo inaweza kuwa na athari kubwa katika kuamua nani ataibuka bingwa wa msimu wa 2024/25.

Pacome amesema ligi imekuwa na ushindani mkubwa, na kila timu inapambana kuhakikisha inapata ushindi ili kufanikisha malengo yake.

“Kila mchezo kwetu ni muhimu na hatuna muda wa kupoteza. Tunajua ushindani ni mkubwa, nasi tunapambana kuwa bora na kupata matokeo mazuri kila tunaposhuka dimbani,” amesema Pacome.

Kiungo huyo pia amesisitiza kuwa ni muhimu kwao kuziheshimu timu zote wanazokutana nazo, hasa katika mzunguko wa pili wa ligi, ambao mara nyingi huwa na ushindani mkali kwani kila timu inahitaji alama muhimu.

Kwa sasa, Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 58 baada ya kucheza mechi 22. Mshambuliaji wao, Prince Dube, pamoja na Clement Mzize, wamefunga mabao 10 kila mmoja, huku Pacome mwenyewe akiwa ametupia mabao saba msimu huu.

Macho yote sasa yanaelekezwa kwenye Kariakoo Derby, ambapo Yanga itakuwa na nafasi ya kujiimarisha zaidi kileleni au kupunguza matumaini yao ya kutetea taji lao.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button