Kwingineko

Omorodion aigomea Chelsea, yahamia kwa Joao Felix

ULAYA: Baada ya dili Chelsea kumnunua mshambuliaji wa Atletico Madrid Samu Omorodion kuota mbawa, taarifa kutoka nchini Hispania zinaeleza kuwa klabu hizo mbili sasa ziko kwenye mazungumzo juu ya uhamisho wa mshambuliaji wao Joao Felix kama mbadala.

The Blues walilenga kumleta darajani ‘fowadi’ Samu Omorodion mwenye umri wa miaka 20 kama mmoja wa washambuliaji wao wakuu mapema mwaka huu.

Mwanzoni, Atletico walikataa kufanya biashara, lakini walilegeza msimamo huo walipojaribu kumnyemelea Conor Gallagher, huku pia wakitaka kumleta fowadi wa Manchester City, Julian Alvarez.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, dili zote tatu zilionekana kuwa na uelekeo wa kukamilika, lakini sasa zote ziko hatarini baada ya uwezekano ya Samu kwenda Stamford Bridge kufifia.

Hapo awali Samu alikuwa amekubali mkataba wa miaka saba Chelsea, lakini ripoti kadhaa kutoka Ulaya zinadai kuwa kulikuwa na shida katika kusaini mkataba huo na uhamisho huu kufa rasmi.

Atletico wanahitaji kufanya mauzo makubwa ili kupata pesa zinazohitajika kwa Gallagher na Alvarez, ambao watagharimu pauni milioni 100. Gallagher tayari yuko Madrid akisubiri uhamisho wake ufanyike, huku Alvarez akiwasili jijini humo baadaye leo Jumatatu kwa vipimo vya afya.

Mwanahabari Fabrizio Romano alikuwa wa kwanza kuripoti Jumapili usiku kwamba Chelsea na Atletico sasa wako kwenye majadiliano juu ya Felix, ambaye alitumia kipindi cha pili cha msimu wa 2022/23 kwa mkopo Stamford Bridge.

Wakala wa Felix, Jorge Mendes, tayari yuko London akiwa amekamilisha kibarua kizito cha kumleta winga wa Wolves Pedro Neto katika viunga vya Stamford Bridge.

Joao Felix alirejea Atletico kwa mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya baada ya kushindwa kupata uhamisho wa kuondoka mazima Wanda Metropolitano.

Felix alicheza Barcelona kwa mkopo msimu wa 2023/24, lakini Atletico haiko katika hali nzuri ya kifedha ya kumrudisha kabisa, wakati huo huo Aston Villa nao wameonyesha nia wiki za hivi karibuni.

Related Articles

Back to top button