Okrah, Skudu, Lomalisa kwisha habari yao!

DAR ES SALAAM. KLABU ya Yanga ipo kwenye mipango ya kuwaacha nyota wao watatu wa kigeni Augustine Okrah, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ na Joyce Lomalisa, ili kupisha wachezaji wengine wapya kwa lengo la kuimarisha timu hiyo ya msimu ujao wa Mashindano.
Nyota wanaotajwa kuchukua nafasi zao ni kiungo mkabaji, Charve Onoya na Agee Basiala wanaokipiga katika klabu ya AS Maniema Union na Chadrack Boka kutoka klabu ya Saint Eloi Lupopo wote kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo {DRC}.
Kabla ya wachezaji hao, tayari Yanga imekubaliana na uongozi wa TP Mazembe ya nchini humo kubadilishana wachezaji huku winga wa kulia Phillipe Kizumbi kutua Yanga na Kennedy Musonda kwenda nchini DR Congo kuchukua nafasi yake.
Taarafa zilizoptika kuwa Yanga wanaendelea kufanya mazungumzo na klabu pamoja na wachezaji hao kwa ajili ya kuimarisha timu yao kwa msimu ujao wa mashindano hasa kufika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa.
“Rais wa Yanga, Hersi Said anaendelea kufanya mazungumzo na klabu walizopo wachezaji hao kwa ajili ya mambo kwenda sawa na kufanikiwa kupata huduma zao na kuja kuziba nafasi ya nyota ambao wanatemwa na kuboresha kwa ajili ya msimu mpya,” amesema mtoa habari huyo.
Kwa mujibu wa Hersi amesema wanahitaji kuboresha zaidi kikosi cha timu yao kwa ajili ya msimu ujao kwa lengo la kufanikiwa malengo yao ya kucheza fainali za Afrika.
Alisema mashabiki na wanachama wanatakiwa kuendelea kuwaunga mkono viongozi, Benchi la ufundi na wachezaji katika mapambano yaliyopo mbele yao ikiwemo fainali ya Kombe la CRDB Bank dhidi ya Azam FC.
“Niwaahidi mashabiki na wanachama tunaenda kujenga timu yetu bora kuliko msimu huu kwa kusajili nyota wengine wenye uwezo na hatutaacha mchezaji yoyote yule ambaye atakuwa kwenye mipango yetu,” alisema Hersi.