Neymar apiga mkwanja mrefu kwa dakika 42 tu juwanjani

RIYADH:Neymar amekuwa na mwaka mgumu wa 2024 uwanjani, lakini licha ya changamoto zake, bado alipokea mshahara mkubwa kutoka kwa klabu yake ya Al-Hilal. Mshambuliaji huyo wa rekodi ya mabao ya Brazil alicheza dakika 42 pekee katika mechi mbili kabla ya mwaka kumalizika, akihangaika kurejea kwenye hali nzuri baada ya jeraha la goti.
Kwa mujibu wa ripoti ya Foot Mercato, Neymar alilipwa takriban pauni milioni 84.6 (Euro milioni 101) kwa mwaka mzima wa 2024, licha ya kutoshiriki ipasavyo. Thamani yake ya uhamisho pia ilishuka sana, kutoka pauni milioni 37 mwishoni mwa 2023 hadi pauni milioni 12.6 mwishoni mwa 2024, kwa mujibu wa Transfermarkt.
Hali hiyo imefanya Al-Hilal kuzingatia kumaliza mkataba wake mapema, huku kukiwa na shaka kuhusu mchango wake katika msimu uliobaki. Mkataba wake wa pauni milioni 130 kwa mwaka unatarajiwa kuisha mwishoni mwa msimu huu.
Endapo mkataba wake utavunjwa, Neymar anaweza kurejea Brazil kujiunga na Santos au kuhamia Inter Miami, ambapo anaweza kuungana tena na Lionel Messi na Luis Suarez, wenzake wa zamani wa Barcelona waliotengeneza utatu maarufu wa MSN.