AFCON

Mwana FA:Tunamuomba radhi Rais Samia

NAIBU Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ amemuomba radhi Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia kufanya vibaya kwa Taifa Stars katika michezo miwili ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya DR Congo.

Stars ilipoteza mchezo wa ugenini bao 1-0 na nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikapoteza mabao 2-0 hapo jana.

Katika mchezo wa kwanza Rais Samia aliisaidia Stars usafiri wa ndege kuhakikisha timu inarudi kutoka DR Congo ikiwa salama na mchezo wa pili alitoa tiketi 20,000 kwa ajili ya mashabiki kuingia bure kuishangilia timu hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, Mwana FA amesema anamshukuru Rais amekuwa akionesha kwa vitendo kuwa ni mwanamichezo namba moja.

“Tunamshukuru Rais amekuwa akionesha yeye ni mwanamichezo namba moja, amekuwa akifanya kwa vitendo. Safari yetu ya mechi iliyopita ya kwenda DR Congo alitoa ndege kuhakikisha timu inarudi na kuwa katika kiwango kizuri. isivyo bahati mechi zote mbili hatujapata matokeo,”

“Tunamuomba radhi mechi zote mbili hatukupata matokeo tuliyokusudia lakini ndio mpira unavyokuwa , timu tuliyocheza nayo inatuzidi sana viwango, hatujapata matokeo lakini tunaanzia hapa tulipoishia, namuahidi tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri mbele ya safari,”ameongeza.

Amesema bado hawajakata tamaa kuna michezo miwili imebaki dhidi ya Guinea na Ethiopia hivyo, watajitahidi kupata matokeo mazuri yatakayowapa nafasi ya kufuzu kushiriki fainali hizo zitakazofanyika Morocco mwakani.

Related Articles

Back to top button