Africa

Mtine: Yanga iko tayari kuivaa Wiliete Benguela

LUANDA: MTENDAJI Mkuu wa Yanga SC, Andre Mtine, amesema kikosi cha Wananchi kiko tayari kwa mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete ya Angola, huku akiwataka mashabiki kuendelea kuwaombea dua njema ili kupata matokeo chanya.

Akizungumza mara baada ya kikosi hicho kutua Angola, Mtine alisema Yanga inakutana na wapinzani wenye hadhi kubwa, kwani Wiliete ni mabingwa wa Angola msimu uliopita, jambo linaloifanya mechi hiyo kuwa na ugumu wake.

“Wapinzani wetu ni mabingwa wa Angola, benchi letu la ufundi limefanya tathmini ya kina juu ya kikosi chao na tunatakiwa kupambana ili kufanya vizuri. Naomba mashabiki watuombee dua njema na naamini tutapata matokeo,” alisema Mtine.

Yanga inatarajia kushuka dimbani kesho katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa na lengo la kuanza vyema safari yake ya kuwania taji la ubingwa Afrika.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga kikosi hicho kitafanya mazoezi jioni ya leo kujiweka imara kwa maandalizi ya mwisho.

Yanga imetoka kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na kuibuka bingwa baada ya ushindi wa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, matokeo yaliyowapa nguvu ya kujiamini kuelekea mchezo huo.

Baada ya mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika watarejea Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano utakaoamua hatma yao ya kusonga mbele.

Related Articles

Back to top button