Msanii wa Mr. Eaz adai muziki wa Ghana hauna faida

GHANA: Msanii wa Ghana J. Derobie amesema kuwa tasnia ya muziki ya Ghana haitoi mapato thabiti hadi msanii afikie kiwango fulani cha mafanikio.
Hitmaker huyo wa ‘Umaskini’ ambaye hapo awali alisajiliwa na lebo ya muziki ya Mr. Eazi ‘Empawa’, alibaini kuwa dhana ya wanamuziki kupata kipato cha uhakika inaweza kuwa ya kupotosha, hasa kwa wale ambao bado hawajaingia kwenye daraja la juu la tasnia hiyo.
“Biashara ya muziki inaweza kuwa na faida kubwa, lakini haihakikishi mapato ya kila siku. Unahitaji kuendelea kufanya kazi na kujisukuma mwenyewe, ” amesema katika mahojiano na Headless YouTuber.
Kulingana na Derobie, kuna kizingiti ambacho wasanii wanapaswa kuvuka ili kufaidika kikamilifu na uwezo wa kifedha wa tasnia ya muziki.
“Kuna mstari maalum wa kuvuka, na mara unapofanya hivyo, ndipo unapoanza kuvuna matunda. Wasanii wengi wenye majina makubwa kama Mr. Eazi, wamevuka mstari huo, na ninaamini ninakaribia kufanya hivyo kwani bila hivyo hakuna faina ya muziki,” ameongeza.
Aidha amesisitiza umuhimu wa uthabiti na kufanya kazi kwa bidii kuwa mambo muhimu yatakayomsaidia kufikia hatua hiyo.
J Derobie pia amekumbuka wakati ambapo malipo ya kifedha kutoka kwa kazi yake ya muziki hayakuja. Kulingana naye, ametamani angerejea kazini kwake ofisini Madina, ambapo ilihakikishiwa kwamba mshahara wake ungelipwa kila mwisho wa mwezi.
“Kuna wakati pesa hazikuwa zikipatikana kutokana na muziki, na kiukweli nilitamani ningebaki kwenye kazi yangu ya ofisini Madina. Angalau pale, nilijua ningelipwa mwishoni mwa mwezi,” J Derobie ameongeza.